WALEMAVU WAKOSA HUDUMA ZA AFYA YA UZAZI

Watu wengi wenye ulemavu wanadaiwa kutopata huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
Hayo yamebainishwa jana jijini Dar es Salaam na mwasilishaji wa madai, Mengi Ntinginyi  kwenye kongamano la 28 la sayansi lililoandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
Katika mada hiyo iliyohusu vikwanzo vya upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa watu wenye ulemavu, alisema utafiti uliofanywa mwaka jana umebaini kundi hilo halipati huduma na linatengwa.
“Pamoja na watu wenye ulemavu kutopata huduma hiyo, lakini wachache ndio wanaojua huduma ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango,” alisema.
Alisema ubaguzi na unyanyapaa katika utoaji huduma ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango kwa watu wenye ulemavu ni moja ya vikwazo vikubwa kwa watu hao kutopatiwa huduma hiyo.
“Watoa huduma wamekuwa wakiwalaumu wanawake wenye ulemavu wajawazito pamoja na wenza wao.
Wanadhani mwanamke mwenye ulemavu hatakiwi kuwa mama.
“Dhana hii inawafanywa watu wenye ulemavu kuogopa kwenda kupatiwa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya afya,” alisema.
Utafauti huo uliofanywa na Maria Stopes Tanzania katika maeneo ya Korogwe, Manispaa ya Lindi, Mtwara na Rufiji.

No comments: