WAKULIMA WA MPUNGA KASULU WALILIA SOKO

Wakulima wa mpunga katika Bonde la Titye wilayani Kasulu mkoani Kigoma, wamesema changamoto kubwa ni soko la uhakika la mazao yao.
Wakizungumza wakati wa ziara ya Balozi wa Ubelgiji nchini, Koen Adama aliyetembelea mradi huo wa kilimo cha umwagiliaji, walisema hali hiyo inawakatisha tamaa.
Wakulima  hao walisema kuwa kutokuwepo kwa soko la uhakika, kumetoa mwanya kwa walanguzi kununua mpunga wao kwa bei ya chini na kuwafanya kutonufaika na jasho.
Katibu wa kikundi hicho cha wakulima, Agatha Mathew alisema bila Serikali kuingilia kati, kutokuwepo kwa soko la uhakika la mpunga, kutawakatisha tamaa wakulima na huenda wakatafuta zao lingine.
Hali hiyo itaipatia hasara Serikali, kutokana na gharama kubwa iliyotumika kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Akizungumzia hali hiyo, Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa Wilaya ya Kasulu, Godian Raphael alisema suala la soko limekumba mazao yote kutokana na kushuka kwa soko nchini Burundi, ambako wakulima hao walikuwa wakipeleka mazao yao.
Hata hivyo alisema kwa sasa bei ya mpunga na mchele, imeanza kuwa nzuri kwa sasa.
Alisema moja ya mambo ambayo wanaomba kwa wafadhili mbalimbali ikiwemo Serikali ya Ubelgiji ni kuomba wasaidie ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao ili kuwepo kwa mtindo wa stakabadhi ghalani, ambao utaondoa walanguzi wanaonunua mazao ya wakulima kwa bei ndogo.
Meneja wa miradi ya umwagiliaji wa Wilaya ya Kasulu, Boniface Burugu alisema tatizo la fedha limefanya miradi mingi ya kilimo cha umwagiliaji, kushindwa kumalizika kwa wakati, hivyo kushindwa kuinua kipato na kuondoa umasikini kwa wakulima wadogo.
Kwa upande wake,  Adams alieleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, ambao umekuwa na manufaa kwa wananchi wenye kipato kidogo.
Aliahidi kuwa nchi yake  itaona namna ya kuweza kusaidia ili kukamilisha mradi huo.

No comments: