WAKULIMA WA MIWA KUPATIWA HATI ZA KIMILA

Serikali kupitia Mpango wa Kurasimisha Rasilimali wa Biashara  (MKURABITA) itatumia zaidi ya Sh milioni 60 kuwapatia wakulima wadogo wa miwa hati za kimila katika vijiji 10 vilivyopo Wilaya za Kilombero na Kilosa  mkoani Morogoro.
Meneja wa Urasimishaji wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara Tanzania (Mkurabita), Makame Juma Pande, alisema  wakulima watakaonufaika na mpango huo  wa kupatiwa hati za kimila ni wa Ruhembe, Kitete Msindazi, Kihelezo na Kidogobasi katika wilaya ya Kilosa.
Vijiji vingine ni Mgombera, Katulukila, Sonjo, Sole, Mkula na Msola Ujamaa vya wilaya ya Kilombero.
Chini ya mpango huo, vijiji 40 katika wilaya za Kilosa na Kilombero vitapatiwa hati miliki za vijiji, ambapo pia hati zaidi ya 5,000 zitatolewa kwa wakulima wadogo wa miwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mkurabita Wilaya ya Kilosa, Symphoroza Mollel, alisema mpango huo utawezesha wakulima kupata mikopo kwa  ajili ya kuendeleza kilimo hicho kwa kutumia hati hizo za kimila.

No comments: