WAKILI ADAI KESI YA MWALE ILIFUNGULIWA KIMAKOSA

Upande wa utetezi kwenye kesi ya wakili maarufu jijini hapa, Median Mwale na wenzake watatu  ya kutakatisha fedha haramu, umedai mashitaka hayo dhidi ya washitakiwa, yalifunguliwa kimakosa kabla ya sheria iliyowashitaki kutungwa.
Kutokana na hoja hiyo, wakili wa upande wa utetezi, Omary Iddi Omary  ameomba kesi hiyo ihamishiwe Mahakama Kuu kupata tafsiri ya kisheria.
Aidha, wakili huyo amelalamikia  kile alichodai ni ucheleweshaji wa makusudi wa kuanza, kusikilizwa kwa kesi unaofanywa na upande wa Serikali kwa kigezo kwamba upelelezi haujakamilika huku wateja wake wakiendelea kusota rumande kwa miaka mitatu sasa.
Alidai hayo jana mbele ya  Hakimu Mkazi Mfawidhi, Devota Kamuzora. Wakili  huyo anasaidiana na Mawakili, Mosses Mahuna na Modest Akida huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Wakili, Tumaini Kweka.
Alidai  kifungu kilichotumika kufungua mashtaka dhidi ya Mwale na wenzake, Elius Ndenjembi, Don Bosco Gichana na Bonifas Mimbwa wanaoshikiliwa kwa muda wa miaka mitatu sasa ni kile kilichofanyiwa mabadiliko Februari 24, 2012, wakati wateja wake wakiwa mahabusu, jambo alilodai kuwa ni kinyume cha sheria.
Omary ambaye aliwasilisha hoja nne tofauti akitaka Mahakama hiyo iwape idhini ya kwenda Mahakama Kuu, alisema hata shtaka lingine walilofunguliwa wateja wake, chini ya Sheria ya Uzuiaji Utakatishaji wa Fedha Haramu ya mwaka 2006, ina upungufu mkubwa kisheria na hivyo si halali.
Alisema  sheria hiyo iliwekwa kwenye Gazeti la Serikali Januari 12, 2006 kabla ya kusainiwa na Rais mwaka  2007, jambo alilodai kuwa linakwenda kinyume na Katiba ya nchi, inayoeleza utaratibu wa kutunga sheria kuwa mara baada ya muswada kupitishwa na Bunge hupelekwa kwa Rais ili aidhinishe kisha itangazwe kwenye gazeti la Serikali ndipo ianze kutumika.
“Mheshimiwa hakimu, kutokana na ukiukwaji wa taratibu hizo, inafanya sheria ya  Utakatishaji Fedha Haramu ya mwaka 2006 isiwepo, hii ina maana hata  washtakiwa  hawa wanashikiliwa kwa kutumia sheria ambayo haipo, hata kosa wanaloshtakiwa nalo halipo kwenye sheria za sasa.’’
Alidai; “ Katika mazingira hayo hakuna shaka kuwa hapa hakuna mashtaka sahihi, na hapa wameweka mtego fulani upande wa mashtaka lakini sisi tunasema tunataka kwenda Mahakama Kuu ili Mahakama hiyo iangalie suala hilo.”
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Tumaini Kweka akijibu hoja hizo alidai hazina msingi kwa madai kuwa sheria hutumika baada ya kupitishwa na Bunge na kuwa imefuata michakato yote.
“Nafikiri wameleta malalamiko kwenye eneo lisilo sahihi, kwani hata kwa mujibu wa uanzishwaji wa Mahakama hii sidhani kama wewe ( Hakimu) unaweza kuamua mashauri ya Manyara, hii ni sawa na kumtuma mtoto akachukue chakula cha mlinzi,” alisema Wakili Kweka jambo lilomfanya Hakimu kuingilia kati na kumtaka afute kauli yake hiyo ya kumfananisha yeye na mlinzi.
Hata hivyo wakili huyo alisisitiza kuwa shauri hilo lipo mahakamani hapo kwa ajili ya kuahirishwa na kupangiwa tarehe nyingine kwa maelezo kuwa Mahakama hiyo haina nguvu kisheria kusikiliza shauri hilo.
“Upelelezi wa kesi hii ni kweli umechukua muda mrefu lakini ikumbukwe kuwa kesi hii ni ya kutakatisha fedha na hakuna sheria inayoweka mipaka ya lini upelelezi uishie ndio maana nimeomba tarehe nyingine lakini wenzangu wamekuja na hoja ya kupinga sheria iliyotumika kuwashtaki washtakiwa. ‘’
Wakili Mahuna alisema kuwa hata wao wanajua kuwa Mahakama hiyo, haina mamlaka kisheria kusikiliza shauri hilo, ndiyo maana wanaomba kupewa idhini kwenda Mahakama Kuu, wakapatiwe ufafanuzi wa kisheria juu ya yale wanayoyalalamikia.
“Tunasikitika kwa upande wa Serikali kila siku kuomba tarehe ya kesi kutajwa, kimsingi haturidhishwi na mwenendo huu, upande wa Jamhuri unatumia mamlaka yake vibaya, tunaomba leo watuambie ni lini hasa upelelezi utakamilika kwani hawaoneshi utayari na hawana hoja ya msingi zaidi ya kauli hiyo kila mara,” alisema Wakili Mahuna.
Hakimu Kamuzora alisema amesikiliza hoja za pande zote mbili na atatoa uamuzi wa awali  Mei 12, mwaka huu.

No comments: