WAFANYAKAZI STRABAG WAENDELEA NA MGOMO WAO

Wafanyakazi wa Kampuni ya ujenzi ya Strabag, wameingia siku ya pili ya mgomo wao huku wakishinikiza kulipwa marupurupu mbalimbali, wanayoyadai kwa zaidi ya miezi saba hadi sasa.
Awali, wakizungumza nje ya ofisi za kampuni hiyo zilizopo Ubungo jijini Dar es Salaam juzi, wafanyakazi hao wanaojenga barabara za mabasi yaendayo kasi chini ya Mradi wa DART, walisema walifikia hatua ya kugoma kwa madai ya kuona wanazungushwa kupewa marupurupu hayo huku wakihofu muda uliobaki kwa kampuni hiyo kabla ya kumaliza kazi yake.
“Marupurupu hayo yanayohusisha fedha za chakula, usafiri, matibabu ambayo jumla yake ni shilingi elfu sabini kwa kila mwezi yapo katika mkataba wa kazi na  mwanzoni tulikuwa tukilipwa lakini cha kushangaza baadaye yalisitishwa bila sababu zozote za msingi,” walisema wafanyakazi hao, ambao hata hivyo hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini.
Kwa mujibu  wao, muda wa kampuni hiyo kumaliza kazi ya ujenzi wa barabara hiyo, unaelekea ukingoni jambo linalowapa hofu ya kupewa malipo hayo huku kesi ya msingi iliyopo mahakamani ikiwa bado haijakwisha wala kujua  itakwisha lini huku wakidai kuendelea kuumizwa na majukumu mbalimbali ya kimaisha.
“Walikimbilia kufungua kesi katika Mahakama ya Kazi ya Kinondoni kutaka kuondolewa kwa malipo hayo, na hadi sasa ni miezi saba kesi bado  ipo mahakamani ikipigwa danadana hatujui lini itakwisha na kama unavyojua karibu wanamaliza kazi tuna hofu haki yetu kupotea,” walisema wafanyakazi hao.
Walisema wakati wao wakifanyiwa kitendo hicho, wafanyakazi wenzao kutoka nchi za Kenya,Kongo na India wanaendelea kulipwa marupurupu hayo kama kawaida huku wakidai kuwa hawaelewi kwa nini wanafanyiwa hivyo wakati kazi wanazozifanya wao zinalingana na wafanyakazi hao wa kigeni.
Wafanyakazi wakiwemo   madereva, waendeshaji wa mitambo, wasimamizi na makundi mengine walisema wanachotaka ni malipo yao bila kujua lini hatma ya kesi iliyotolewa itafikiwa vinginevyo  hawatokuwa tayari kurejea kazini.
Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jordan Rugimbana amewataka wafanyakazi hao kurejea kazini wakati suala lao likiendelea kushughulikiwa na mamlaka zinazohusika.
Akizungumza na mwandishi jana, alisema baada ya kupata taarifa hizo juzi, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, uongozi wa Strabag, viongozi wa wakala wa Barabara nchini (TANROADS) pamoja na viongozi wa Ofisi ya DART walikutana kuzungumzia suala hilo alilosema kuwa hata hivyo linahitaji busara kwa kuwa kesi yake bado ipo mahakamani.

No comments: