VODACOM TANZANIA WAENDA 'PEMBEZONI' MWA NCHI

Kampuni ya Vodacom Tanzania imechaguliwa kuwa moja ya watoa huduma za mawasiliano watakaotoa mawasiliano ya simu vijijini na mijini ambayo awali haikupewa kipaumbele.
Katika kufanikisha hilo, kampuni hiyo imesema inatarajia kufikia wakazi takribani milioni moja wa maeneo husika.
Taarifa iliyotolewa na kampuni hiyo jana kwa vyombo vya habari, imemkariri Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Rene Meza kisema wameshinda zabuni ya kutoa huduma za mawasiliano ya simu kwa vijiji 466 katika kata 73 ambazo zina wakazi takribani 1,000,000.
“Haya ni mafanikio makubwa kwetu sisi kuendelea kuwatumikia watanzania kwani inaonesha jinsi  mtandao wetu unaaminika. Vodacom  ipo mstari wa mbele kushirikiana na serikali pamoja na taasisi za kimataifa kuhakikisha wateja wake wanafikiwa kila pembe ya nchi,” alisema.
Alisema nchi bado ina uhitaji mkubwa wa huduma za mawasiliano na ni jukumu lao kuwahudumia.
Zabuni hiyo ilitolewa na  mfuko wa kimataifa wa kutoa huduma za mawasiliano (UCSAF) ikiwa ni sehemu ya mpango wa miundombinu ya mawasiliano Tanzania na mfumo wa kielektroniki wa serikali  (RCIP-Tanzania) ambao umefadhiliwa na  taasisi ya kimataifa ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini  makubaliano hayo kwa kampuni za simu za mkononi ambazo zimeshinda zabuni za kutoa huduma za kimawasiliano vjijini,  Mtendaji Mkuu na Meneja wa Mfuko wa UCSAF, Peter Ulanga alisema walitangaza zabuni hiyo kwa kata 152 ambapo zitawafikia watu takribani 1,600,000.
Kwa mujibu wa Ulanga, mshindi wa zabuni hiyo amepatikana kwa kufuata taratibu zote kwani kulikuwa na fursa sawa kwa kila kampuni.
UCSAF ilianzishwa kwa lengo la kukuza upatikanaji wa teknolojia ya habari na mawasiliano duniani kote.

No comments: