VIZIWI BUGURUNI KUPATIWA VIFAA VYA TEHAMA

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote umeipatia Shule ya Msingi Buguruni Viziwi msaada wa vifaa vya Tehama na huduma ya mtandao wa intaneti, vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 16 kwa ajili ya kufundishia shuleni hapo.
Buguruni Viziwi ni miongoni mwa shule 10 zitakazonufaika na vifaa hivyo vya Tehama, ambavyo ni pamoja na kompyuta 10 na meza zake na vifaa vingine vya  Tehama kulingana na mahitaji maalumu ya shule husika.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Peter Ulanga, alisema mfuko pia umelenga kuunganisha shule 25 za umma kwa mtandao wa intaneti,  mradi utakaofadhiliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa ushirikiano na kampuni ya Mawasiliano ya Avanti.
Ulanga alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa kuunganisha shule 25 za umma kwa mtandao wa intaneti, uliofanywa shuleni hapo.
Mgeni rasmi  katika hafla hiyo, alikuwa ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dk John Mngodo.
Shule zilizoainishwa  kwenye mradi huo ni shule za msingi Buguruni Viziwi, Uhuru Mchanganyiko, Mbuyuni, Kisiwandui, Mpilipili Maalumu, Manyoni, shule ya mazoezi ya kufundishia Patandi, Dumila na shule ya Mtanga Maalumu. 
Mwalimu Mkuu wa shule ya Buguruni Viziwi, Winfrida Jeremiah amesema  ukosefu wa umeme wa Tanesco mara kwa mara, upungufu wa walimu wenye ujuzi wa kompyuta na ukosefu wa ubora wa chumba cha kompyuta  ni changamoto zinazoikabili shule yake.
Aliomba Serikali kuwasaidia kupata umeme wa jua, marekebisho ya chumba cha matumizi ya kompyuta na walimu wapewe mafunzo ya kutumia mitandao kompyuta. Buguruni Viziwi ina wanafunzi 271 kati yao wavulana ni 135 na wasichana 136.

No comments: