'VIJANA ACHENI KULALAMIKA, JIUNGENI MSAIDIWE'

Vijana mkoani Lindi wametakiwa kuacha tabia ya kuilalamika Serikali kuwa maisha ni magumu bali watumie fursa zilizopo katika maeneo yao kujiajiri na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.
Mwito huo umetolewa jana na Mjumbe wa Baraza kuu na Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCC) Taifa kutoka mkoa wa Lindi, Jabir Makame kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mnazi mmoja wilaya ya Lindi Mjini.
Mkutano huo ulikuwa ni wa kuzipokea mbio za kizalendo za pikipiki na kuwaelimisha wananchi umuhimu wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Halmashauri zetu zinatakiwa kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya kinamama na vijana naamini hata halmashauri za mkoa huu zinafanya hivyo lakini fedha hizo hazitolewi kiholela ni lazima wahusika wajiunge  katika makundi yaliyosajiliwa  kwa mfano  kundi la madereva wa bodaboda, bajaji, kina mama lishe na vikundi vya mpira pia vinaweza kuwa vya ujasiriamali na kuweza kupata mkopo ambao watautumia katika shughuli zao za maendeleo", alisema Jabiri.
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu Taifa (MNEC) wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo aliwapongeza UVCCM kwa kuandaa mbio hizo za uzalendo kwani ni ukweli usiopingika kuwa Muungano wenye dhana ya kizalendo na historia ya nchi unatimiza miaka 50 ifikapo Aprili 26 mwaka huu.
Mama Kikwete alisema, "Leo hii nchi kubwa zenye nguvu kiuchumi duniani zinazungumzia suala la kuungana ili kuimarisha nguvu yao ya pamoja, kwa nini sisi tukubali kutengana? Muungano wetu ni kigezo kizuri ndani ya Bara la Afrika  na kote Duniani tusikubali kamwe kuuvunja jambo kubwa hapa na la msingi ni kukaa kwa pamoja na kujadili hatimaye kupata ufumbuzi yakinifu".
UVCCM mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara waliandaa mbio za uzalendo za pikipiki zenye kauli mbiu Miaka 50 ya Muungano Dumisha Muungano, vijana tutumie fursa zilizopo katika maeneo yetu. Tanzania kwanza mengine baadaye ambazo zilizinduliwa mkoani Ruvuma katika wilaya ya Namtumbo Aprili 13, 2014 kumalizika mkoani Lindi tarehe Aprili 17, 2014.
Mkoa wa Lindi ulizipokea mbio hizo kutoka kwa vijana wa Mtwara makabidhiano yaliyofanyika kata ya Madangwa.
Lengo la mbio hizo ni kuwaenzi waaasisi wa Taifa la Tanzania  ambao ni Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amaan Karume Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kuwafikishia ujumbe watanzania  juu ya umuhimu wa muungano na kuwaeleza wapi ulipotoka, ulipo na unakokwenda na vijana kutumia fursa zilizopo kujiendeleza.

No comments: