VIGOGO WATEGWA AJIRA ZAO VIWANJA VYA NDEGE

Uchochoro wa dawa za kulevya katika viwanja vya ndege nchini, umegeuka shubiri ambapo sasa nafasi za vigogo wa Bodi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) zimegeuka za moto.
Hali hiyo imesababishwa na aibu iliyokwishatokea kwa Taifa, iliyotokana na kukamatwa kwa dawa za kulevya katika viwanja vya ndege vya kimataifa, zikionekana kwamba zimepita katika viwanja vya ndege vya hapa nchini.
Jana Rais Jakaya Kikwete, alitoa mwezi mmoja kwa viongozi wa  TAA, kuweka mifumo imara ya usalama katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na wasipotekeleza atawachukulia hatua.
Alisema hayo wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa jengo jipya la abiria, kituo cha tatu, cha JNIA ambalo pamoja na fursa zingine za kibiashara, litachochea ajira mpya zaidi ya 7,000.
Rais Kikwete alionesha wazi kutoridhishwa na hali ya usalama katika viwanja hivyo, na kuonya kuwa atawawajibisha viongozi wa TAA wasipotekeleza agizo hilo, ikiwemo kuwafukuza kazi wafanyakazi wote wanaotiliwa shaka kuhusika kupitisha dawa za kulevya.
Rais Kikwete aliweka wazi kuwa ataanza kumwajibisha Mkurugenzi wa TAA, Suleiman Said Suleiman na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi hiyo, Lambert Ndiwaita, wasipotekeleza agizo hilo.
Alisema kuwa maagizo anayotoa Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, kuhusu usalama wa viwanja hivyo ni maagizo yake hivyo yasipotekelezwa atawachukulia hatua.
"Suleiman (Mkurugenzi wa TAA), nataka ufahamu kuwa maagizo yanayotoka kwa Mwakyembe ni yangu, usipotekeleza nitaanza na wewe na Mwenyekiti wako wa Bodi kwani nasononeka sana na hali hiyo ya kuacha wanamuziki wakipita na dawa za kulevya  huku wakiwaimbia," alisema Rais Kikwete.
Pia aliomba apelekewe majina ya wafanyakazi wanaotiliwa shaka kupitisha dawa hizo, ili awafukuze kazi yeye mwenyewe kwa kuwa mamlaka hayo ya kuwaondoa bila kuwaonea haya anayo, na hakuna mtu atakayemuuliza wala kumshitaki.
Alisema haiwezekani kuendelea na hali hiyo ambayo  inamuumiza na ikiwa watendaji hao hawaumii, watachukuliwa hatua. 
Amesema kitendo cha dawa za hizo kupita JNIA na KIA na kukamatwa katika nchi nyingine, kinasababisha Watanzania wote kuonekana wanafanya biashara hiyo.
"Tusifanye masihara na usalama wa kiwanja chetu kwani kikiwa njia ya kupitisha dawa za kulevya, tunaaibisha nchi yetu pamoja na Watanzania wote.
"Hii siyo nzuri, mnaenda mbele na kurudi nyuma (katika usalama), ni afadhali kuanza sasa na siyo kuamua kila siku bila utekelezaji na sisi wote kuonekana tunafanya biashara hiyo," alisema Rais Kikwete.
Alihadharisha kuwa Sheria ya Manunuzi isiwe kisingizio cha kuchukua miaka miwili bila utekelezaji, kwani ikiwa sasa abiria wanaopita katika kiwanja hicho ni milioni 2.5 wanashindwa kuwadhibiti, itakuwaje kikikamilika kipya na kufikia milioni sita kama sio kuwa biashara huru ya dawa za kulevya?
Alisisitiza ni vema mfumo huo wa usalama ukaanza na JNIA na KIA ambako kumeonekana kuwa uchochoro wa kuingiza dawa za kulevya nchini na kuhadharisha kuwa udhibiti ukifanyika JNIA pekee, wafanyabiashara hao haramu watakimbilia KIA.
Rais Kikwete alisema kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha tatu, kutatoa fursa ya ukuaji wa uchumi kufikia wa kati ifikapo 2025 kwani kutakuwa na ongezeko la idadi ya ndege, abiria na ongezeko la safari za ndani na nje ya nchi.
Alisema usafiri wa anga kwa sasa siyo anasa, bali msingi wa usafiri huo ni kuwa wa haraka na uhakika na pia ni mhimili mkubwa katika sekta ya utalii na biashara.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, watalii wengi wamekuwa wakishindwa kufika katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na gharama kubwa ya usalama.
Alisema hata gharama za usafiri huo kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, ni mara mbili ya nchi za Ulaya kwa safari ya saa sita hivyo uwanja huo mpya utasaidia kuboresha huduma, kuongeza biashara na kutokana na ongezeko la watu watakaotumia uwanja huo, nauli itapungua.
Alisema atahakikisha Hazina wanasaini fedha zinazotakiwa haraka, ili jengo hilo likamilike kwa muda uliopangwa.
Awali akizungumzia ujenzi wa kituo hicho, Suleiman alisema ujenzi wa jengo hilo lenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni sita kwa mwaka na miundombinu yake, linatarajiwa kugharimu Sh bilioni 518 mpaka kukamilika.
Alisema mradi huo, unatekelezwa kwa fedha za mkopo kutoka benki ya HSBC ya Uingereza kwa dhamana ya Serikali ya Uholanzi kupitia taasisi ya Atradius na benki ya CRDB.
Suleiman alisema jengo hilo litakuwa na ukubwa wa meta za mraba 70,000, sawa na mara nne ya jengo lililopo sasa lenye ukubwa wa meta za mraba 15,000 na limeanza kujengwa Januari mwaka huu na linatarajia kukamilika Oktoba mwakani.
Mbali na kuchochea fursa za ajira kwa Watanzania wapatao 7,000, pia jengo hilo na miundombinu yake, itatoa fursa ya kuegesha ndege aina zote ikiwemo ndege kubwa kwa sasa duniani ya A380.

No comments: