VIGOGO TANESCO KORTINI KWA HASARA YA MILIONI 275/-

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imewafikisha mahakamani vigogo wanne wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na msambazaji kutoka kampuni ya M/S Young Dong Electronic Co. Ltd, kwa tuhuma za kuisabishia Serikali hasara ya Sh milioni 275.
Vigogo hao ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Robert Semhilu, Ofisa Ugavi, Harun Mahambo, Mkurugenzi wa Fedha, Lusekelo Kasanga na Mwanasheria wao, Godson Makia pamoja na msambazaji Martin Simba.
Hata hivyo Makia ndiye aliyepandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka hayo jana, huku Mahakama ikitoa hati ya kukamatwa kwa washitakiwa wengine ili wafikishwe mahakamani hapo kusomewa mashitaka yanayowakabili.
Wakili kutoka Takukuru, Isidol Kyando  alidai mbele ya Hakimu Mkazi Hellen Liwa kuwa, Desemba 2011 katika ofisi za Tanesco Ubungo, Makia na wenzake wakiwa waajiriwa wa shirika hilo, walitumia madaraka yao vibaya kwa kufanikisha malipo kwa msambazaji Martin Simba bila ya kufanya uhakiki.
Kyando alidai washitakiwa hao walifanya hivyo kinyume na kifungu namba 35 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma jambo lililosababisha msambazaji huyo kupata faida.
Aliendelea kudai kuwa kati ya Januari na Desemba, mwaka  2011 katika ofisi za Tanesco Ubungo, washitakiwa hao wakiwa waajiriwa wa shirika hilo pamoja na msambazaji huyo waliisababishia Serikali  hasara ya Sh 275,040,000.
Mshitakiwa alikana mashitaka na kurudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa fedha taslimu Sh milioni 27.5, na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, mmoja awasilishe hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo.
Kyando alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika ambapo Hakimu Liwa aliahirisha kesi hadi Aprili 30 mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa na kuangalia kama washitakiwa wengine watakuwa wamekamatwa ili wasomewe mashitaka yao.

No comments: