VETA KUPIMA VYUO KWA KUANGALIA WANAOJIAJIRI

Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) imesema wataanza kuvipima vyuo vyake binafsi kwa kuangalia idadi ya wahitimu wanaojiajiri na kuajiriwa huku wakisema somo la ujasiriamali ni lazima katika vyuo hivyo.
Aidha, ili kufikia malengo yake Mamlaka hiyo imeanza  mawasiliano na Mfuko wa Vijana wa Manispaa na Taasisi za kibenki kuwapatia mitaji vijana wanaohitimu katika vyuo vyake.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Kanda ya Dar es Salaam, Bernadeta Ndunguru alisema hayo jana wakati wa kongamano la wakuu na wamiliki wa vyuo vya ufundi stadi katika kanda hiyo.
Alisema ili kupata mitaji, mamlaka imefanya mazungumzo na Mifuko ya Vijana katika manispaa na wamewaelekeza namna ya kufanya pamoja na Benki ya Wananchi wa  Dar es Salaam (DCB) ambayo iko tayari kufanya kazi na VETA.
Alisema  katika kuvipima vyuo hivyo wamewataka kuunda vitengo maalumu ambavyo vitakuwa na kazi ya kufuatilia waajiri na kupeleka wanafunzi wao katika masomo ya vitendo kuwaunganisha na waajiri.
Akifungua kongamano hilo, Mkurugenzi wa Mradi wa kuwajengea uwezo Vijana, ujulikanao kama Tanzania Youth Scholars (TYS), Sarah Shebele unaofanywa kwa kushirikiana na VETA alisema vyuo binafsi  vinatakiwa kuwa na vitendea kazi kwa ajili ya kuwezesha vijana kupata ajira.

No comments: