UTPC, UINGEREZA KUPIGA VITA VIFO VYA WAJAWAZITO

Serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Muungano wa Klabu za  Waandishi wa Habari Tanzania(UTPC), watashirikiana na jamii vikiwemo vyombo vya habari hapa nchini, katika kupigania afya ya mama na mtoto ili kupunguza vifo,  vinavyojitokeza mara kwa mara.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeshauriwa kutoa kipaumbele cha bajeti ya huduma za afya nchini kuielekeza vijijini, kutokana na takwimu kuonesha asilimia 78 ya wanawake wanaojifungua hutoka vijijini badala ya mijini.
Hayo yamebainishwa kwenye warsha ya waandishi wa habari kutoka mikoa yote ya Tanzania, iliyofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia mradi wake wa Evidence for Action.
Mkurugenzi wa E4A,Craig John Fela, alieleza katika warsha hiyo kuwa, takwimu za vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini Tanzania ni miongoni mwa sababu zilizoisukuma Serikali ya Uingereza kupitia mradi wake wa maendeleo DFID kwa kushirikiana na UTPC kupambana na vifo vitokanavyo na uzazi.
Alisema takwimu zinaonesha wanawake wajawazito 8,500 hupoteza maisha kila mwaka, huku watoto wachanga 48,000 chini ya mwezi mmoja wakifariki dunia kutokana na uzazi.
Hata hivyo alisema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya habari kuwa ni hazina katika kuhamasisha mabadiliko na kuelimisha jamii katika kupambana na vifo hivyo; kuna haja kwa sekta hiyo kutoa kipaumbele cha habari za afya ili jamii iweze kutambua tatizo lilivyo kubwa na kuchochea mabadiliko ya haraka.
Kadhalika itasaidia baadhi ya viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wa vijiji, kutambua umuhimu wa kushirikiana na jamii katika mkakati madhubuti wa kutokomeza vifo hivyo.
Rais wa UTPC, Keneth Simbaya alisema kila mwananchi anawajibu wa kulinda afya ya mama mjamzito na mtoto kutokana na ukweli kwamba kila binadamu kazaliwa na mwanamke na kupita hali ya kuwa mtoto.
Iwapo jamii itaelimika ipasavyo, vifo hivyo vina uwezo mkubwa wa kuepukika hatua itakayoongeza uwajibikaji katika kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Aidha waandishi wa habari wanapaswa kutumia taaluma yao vizuri ili kuchochea kueleza faida ya wajawazito kujifungulia kwenye vituo vya afya.

No comments: