USHIRIKINA WASHUSHA UFAULU SHULENI KANDA YA KATI

Imani za kishirikina, maagizo ya wazazi kwa watoto wao kuhusu kujiendeleza kumeelezwa kuwa chanzo kikubwa cha kushuka kiwango cha ufaulu shule za msingi na sekondari Kanda ya Kati.
Changamoto hizo zimeelezwa katika kikao cha tathmini ya ufaulu wa shule za sekondari Kanda ya Kati kinachofanyika mjini Dodoma.

Kikao hicho kinawahusisha wakuu wa shule za sekondari za Kanda ya Kati.
Mkuu wa Sekondari Sakami iliyopo wilayani Kondoa, Damas Mshanga, alisema kuwa changamoto kubwa shuleni kwake ni imani za ushirikina.
Alisema walimu wengi wanaopangiwa kufundisha kwenye wilaya hiyo wamekuwa wakikimbia shule kwa madai ya kufanyiwa mambo ya kishirikina.
"Kibaya zaidi pamoja na baadhi ya wanajamii kudaiwa kujihusisha na
ushirikina huo hata wanafunzi nao wamekuwa wakihusishwa pia," alisema
Mshanga ambaye pia aliongeza kuwa walimu mara nyingi wameripoti kushushwa vitandani mwao na kulazwa chini bila wenyewe kujitambua.
Alisema kukosekana kwa walimu kumefanya shule yake kuwa ya mwisho kikanda.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Kisana, Iramba mkoani Singida, Elly Nguma alisema changamoto nyingine inayochangia kuporomoka kwa ufaulu huo ni pamoja na wanafunzi wanaochaguliwa kidato cha kwanza kutojua kusoma na kuandika.
"Wengi wanaochanguliwa kuingia kidato cha kwanza hawajui kusoma na
kuandika, jambo ambalo limekuwa ni tatizo kubwa la kupata ufaulu mzuri
kwenye shule nyingi zilizopo kwa Kanda ya Kati," Nguma alisema.
Aidha wazazi na walezi baadhi yao pia wamekuwa sababisho la kuwa na matokeo mabaya ya elimu kwa kuwafundisha watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao hata kama wanayafahamu majibu.
Elly aliongeza kusema kuwa pia utoro pamoja na kuacha masomo kwa malengo ya kukimbilia mijini kwa nia ya kutafuta ajira, nayo imechangia kwa kiasi kikubwa cha kushuka kwa kiwango cha ufaulu katika masomo wanayofanya.
Aidha baadhi ya wazazi na walezi wenye mifugo pia wamehusika katika
kuporomoka kwa elimu, kutokana na watoto wao wanaporudi nyumbani wanatumia muda mwingi kuchunga mifugo badala ya kujisomea.
Kwa upande wake Mkaguzi Mkuu wa Shule Kanda ya Kati Regina Arevo, alikiri kushuka kwa kiwango hicho na kudai kuwa kimechangia kwa kiasi kikubwa na jamii kujihusisha na imani hizo za kishirikina.
Regina alisema kuwa katika Kanda ya Kati baadhi ya shule ziko nyuma
kitaaluma kwa wanafunzi ndiyo maana wakabuni mpango huu wa kuwashirikisha shule zilizofanya vizuri na zilizofanya vibaya katika ufaulu.

No comments: