USHIRIKIANO WATAKIWA KUBAINI WAHAMIAJI HARAMU

Jamii imetakiwa kutoa ushirikiano katika kuwabaini wahamiaji haramu, waliojipenyeza kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo, itasaidia kupata viongozi ambao ni raia halisi wa hapa nchini.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji Wilaya ya Shinyanga, Salumu Farahani alisema wahamiaji haramu wanapochaguliwa kuwa viongozi, sio wazalendo na hawana uchungu na nchi hii. Aliwataka wananchi, kuchagua mtu ambaye wanajua historia yake.
Farahani alisema kumekuwepo na wimbi la wahamiaji, ambao wamekuwa wakiishi nchini kinyume cha sheria na jamii kushindwa kuwafichua.
Kamishina huyo aliitaka jamii kuwabaini  wahamiaji haramu katika maeneo yao, kuepusha madhara ya kupata viongozi ambao sio wazalendo, kwa kuwa na uraia wa nchi nyingine, hali ambayo inaweza kuzorotesha maendeleo  ya Taifa.
“Changamoto tunazo kumbana nazo  katika kuwabaini wahamiaji haramu ni kukosekana kwa uwazi na ushirikiano kwa jamii, hii ni changamoto kubwa kwa kuwa wao ndiyo wanaishi nao; lakini wanashindwa kuwa
wazi,tunaiomba jamii itusaidie tukomeshe tatizo hili,” alisema.
Pia, alisema katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba mwaka jana, walifanya msako na kukamata wahamiaji haramu 18 kwenye wilaya hiyo.
Alisema wengi wa watu hao, walishaweka makazi miaka mingi, hivyo kuwa vigumu kuwarejesha katika nchi zao kwa kuwa hawatambuliki.
Farahan alisema kutokana na changamoto hiyo, wameanza kuelimisha jamii ili wapate vitambulisho vya uraia na kuishi kwa mujibu wa sheria za nchi.
Alisisitiza kuwa ushirikiano na uwazi, ndiyo njia pekee  itakayomaliza tatizo la watu kuhamia kutoka nchi nyingine na kuishi kinyemela.
Aliongeza kuwa raia wa kigeni wengi wanaokamatwa ni kutoka Rwanda ndio inaongoza na kufuatiwa na Burundi pamoja na Uganda.

No comments: