USAFIRI WA 'TRENI YA MWAKYEMBE' WABAKIA KITENDAWILI

Majaliwa ya kurejea kwa usafiri wa treni inayofanya safari zake kati eneo la Stesheni hadi Ubungo yamebaki kuwa kitendawili tangu treni hiyo ilipositisha huduma zake wiki moja iliyopita baada ya kuacha njia ghafla.
Hatua hiyo inachangiwa na kutokuwepo kwa taarifa zozote kutoka kwa kwa uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL)kwenda kwa wananchi, hatua ambayo mbali na mambo mengine inasababisha usumbufu kwa watumiaji wa usafiri huo.
Hata hivyo, msemaji wa kampuni hiyo Midladjy Maez aliliambia gazeti ili kupitia ujumbe mfupi wa simu, kuwa taarifa za kurejea kwa usafiri zitatolewa mara baada njia za treni hiyo kukamilika.
Mbali na kuacha njia kwa kichwa hicho pia utelezi uliokuwepo katika eneo la Gerezani, ulisababisha mabehewa ya treni hiyo kuanguka hatua iliyowatia hofu wananchi kuhusu usalama wa treni hiyo hususani katika kipindi hiki cha mvua.
Kusimama kwa huduma za treni hiyo kwa kiasi kikubwa kumewaathiri wananchi kutokana na shida ya usafiri inayolikabili Jiji la Dar es Salaam kwa sasa inayosababishwa na msongamano mkubwa wa magari pamoja na ubovu wa miundombinu.

No comments: