Ukawa wafungasha virago Bunge la Katiba

Baada ya kushindwa kwa upotoshaji uliofanywa na wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), linaloongozwa na Chadena na CUF na hoja zao kuanza kupoteza mwelekeo, wajumbe hao wameamua kufungasha virago kurejea makwao kujipanga kutafuta huruma ya wananchi.

Wajumbe hao wamefikia uamuzi huo jana, baada ya kukaa Dodoma na kuchukua posho za siku zote za awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu mpaka Aprili 30 mwaka huu, walizozitumia pamoja na mambo mengine kukashifu waasisi wa Muungano uliodumu kwa miaka 50 sasa, Mwalimu Julius Nyerere na Shekhe Abeid Amaan Karume.
Hatua hiyo ya Ukawa pia imefikiwa baada ya Hati ya Muungano kuwasilishwa bungeni, ambayo imewaumbua kwa kuwa kwa siku zote walizokuwepo wajumbe hao Dodoma, walikuwa wakisema hati hiyo haipo na hivyo Muungano uliodumu kwa miaka 50 sasa ni batili, ili kuvuruga muundo wa serikali mbili uliopo sasa kwa kuunda serikali tatu.
Hali hiyo ilianza tangu Kamati 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zilipoanza kazi ambapo wajumbe hao wa Ukawa, walitishia kuvuruga Bunge hilo, kwa madai kuwa hawawezi kujadili hoja ya Muungano wakati Hati ya Muungano iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere na Shekhe Karume haipo.
Walipewa Sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano, iliyothibitisha Muungano huo iliyosainiwa na Mwalimu Nyerere, Spika wa Bunge Adam Sapi Mkwawa na Katibu wa Bunge wakati huo, Pius Msekwa.
Hata hivyo, wajumbe hao wa Ukawa walidai sahihi za viongozi hao zimeghushiwa na hata Msekwa alipofika kuwahakikishia kuwa ni sahihi yake, waliikataa na kuendelea kupotosha umma kuwa Muungano ni batili kwa kuwa hati za Muungano hazipo.
Baada ya taarifa za Kamati za Bunge kuanza kujadiliwa, wajumbe wa Ukawa, wakiongozwa na msemaji wao Tundu Lissu, waliendelea kujenga hoja zao kwa nia ya kubatilisha Muungano kwa kutumia upotoshaji kuwa Hati ya Muungano, haipo.
"Swali la msingi linalohitaji kuulizwa, je, hati hii ipo? Swali la pili, je, hati hii ni halali? Swali la tatu, kama hati hii ipo na ni halali je, Muungano huu ni halali?" Alisema msemaji wa Ukawa, Tundu Lissu, alipokuwa akianza kujenga hoja ya kuvunja Muungano kupitia madai ya kutokuwepo kwa Hati ya Muungano.
Lissu alisema hakuna ushahidi kwamba kuna Hati ya Muungano kwa kuwa hata Umoja wa Mataifa, kunakoelezwa ilipelekwa, wamethibitisha hakuna jambo hilo.
"Hati ya Muungano haipo Zanzibar wala Tanganyika, haipo UN wala bungeni, sasa hiki kilichozungumzwa na wengi kuwa kuanzisha muundo wa serikali tatu ni kuvunja hati hizo ni uongo tu, zama za uongo sasa zimefikia mwisho.
"Nusu karne ya uongo sasa ikome, tuambiane ukweli hivi sasa, waliozoea vya kunyonga kamwe hawawezi vya kuchinja, mimi nawataka wajumbe wenzangu tufikie mwisho wa kudanganya.
"Ni nani aliyeshuhudia wakati wa kutiliana saini makubaliano ya Muungano? Hakuna walioshuhudia, wale wote walioshuhudia jambo hilo waliuawa, sasa mnahofia nini kuingia kwenye serikali tatu?" alisema Lissu huku akiwakashifu waasisi wa Muungano huo.
Kutokana na hatua hiyo, Rais Jakaya Kikwete, aliagiza Hati ya Muungano, iwekwe hadharani na waandishi wa habari wakawa wa kwanza kuishuhudia ambapo aliagiza pia iwekwe katika Makumbusho ya Taifa, ili Mtanzania yeyote aione na ipelekwe katika Bunge Maalumu, ambako Ukawa wamekuwa wakipotosha kuwa haipo.
Akionesha Hati halisi ya Muungano mwanzoni mwa wiki hii, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, alisema Rais Kikwete ameridhia nakala zilizothibitishwa kisheria, ziwekwe kwenye Makumbusho ya Taifa ili kila mwananchi aione na kuepuka upotoshaji huo.
Akizungumzia ilipokuwa hati hiyo, Balozi Sefue alisema hati hiyo ipo, ilikuwepo siku zote na kufafanua kuwa ni lazima baadhi ya hati muhimu zihifadhiwe kama mboni ya jicho.
"Lazima tukubaliane kuwa zipo hati fulani ambazo ni kiini cha uwepo wetu kama Taifa huru, Jamhuri huru na Muungano huru, ambazo tunazihifadhi kama mboni ya jicho.
"Hati hizo ni pamoja na Hati ya Uhuru wa Tanganyika ya mwaka 1961, Hati ya Tanganyika kuwa Jamhuri mwaka 1962, na Hati ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964.
"Hati za aina hii zinahifadhiwa maeneo maalum ambayo ni salama ili zisipotee wala kuharibika. Kwa kawaida hatuzitoi, tunazihifadhi kwa namna yoyote ile," alisema Balozi Sefue.
Baada ya Hati hiyo kuoneshwa kwa wanahabari na kupelekwa bungeni kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kwa faksi, Ukawa walijikuta katika hali ngumu kuendeleza hoja zao kwa kuwa kiini cha kubatilisha Muungano, kuunda serikali tatu, kilikuwa upotoshaji wa kutokuwepo kwa Hati ya Muungano.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, alilazimika kumtetea Lissu kwamba alilazimika kusema kuwa Hati hiyo haipo, kwa kuwa viongozi wengi na tume nyingi zilitaka kuiona bila mafanikio.
Ili kuongeza nguvu katika upotoshaji huo, Mbowe alidai kuwa bado hawana hakika na saini za Mwalimu Nyerere na Shekhe Karume, mpaka zitakapochunguzwa na taasisi za kimataifa.
Mbowe alijikuta akijichanganya aliposema; "Hati iwepo isiwepo Muungano ni muhimu ila ujengwe katika misingi ya kweli, uwazi na haki," wakati Lissu ndiye aliyekuwa akisema uongo kuwa hakuna Hati ya Muungano.
Jana Hati ya Muungano iliyothibitishwa kisheria, iliwasilishwa bungeni huku wajumbe wa Ukawa waliodai kuwa watataka kuihakiki, wakipewa ruhusa kwenda katika taasisi yoyote ya kimataifa kuchunguza uhalali wa Hati ya Muungano.
Taarifa ya kuwasilishwa kwa hati hiyo bungeni, ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya  Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira, baada ya kutakiwa kufanya hivyo na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samia Suluhu.
"Nasimama katika Bunge lako tukufu, nikiliambia na kuwaambia Watanzania, Hati ya Muungano iliyokuwa inapigiwa kelele sana ipo na tena ipo katika hali nzuri tangu iliposainiwa miaka 50 iliyopita.
"Nafurahi kwamba hati hiyo ipo na imewasilishwa ndani ya siku mbili ikiwa katika nakala iliyothibitishwa kisheria na salama kama tulivyosema nachotaka niseme sisi sote tumeapa hapa na mwisho wa kiapo chetu, tulisema ewe Mungu nisaidie.
"Juzi (Jumatatu) nilisema hati ipo hata kabla ya kuileta hapa, hii ina maana Muungano ulikuwepo hata kabla ya hati, maisha ya Watanzania hayapo ndani ya vipengele vya sheria, tumeleta hati ili uongo na ukweli vijitenge, tena imepigwa chapa ya zamani na kama hawaamini, waichukue waipeleke nje (ya nchi) kuichunguza.
"Hata sisi tukiipeleka huko, watasema wataalamu walioichunguza wamehongwa," alisema Wasira akizungumza na mwandishi nje ya ukumbi wa Bunge.
Hoja kubwa ya Ukawa ya kutokuwepo kwa Hati ya Muungano, iliyokuwa msingi wa kutetea muundo wa serikali tatu zilipoanza kukosa mashiko, waliamua kuanza kuwakashifu waasisi wa Muungano.
Hatua hiyo ya Msemaji wa Ukawa, Lissu, kwa niaba ya kundi lake kuwatukana waasisi wa Muungano,  iliamsha hisia za jamii na za kisiasa dhidi ya Ukawa kabla ya kundi hilo kuamua ghafla kufungasha virago.
Kwanza alianza Mufti Mkuu wa Zanzibar, Alhaji Shekhe Saleh Kabi, ambaye alikemea matusi na kauli za kebehi kwa viongozi wakuu wa nchi na waasisi wa Taifa zinazotolewa na wajumbe wa Bunge Maalumu  linaloendelea huko Dodoma.
Shekhe Kabi alisema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamekabidhiwa majukumu makubwa ambayo lengo lake ni kupata Katiba mpya yenye maslahi kwa wananchi wote.
Kauli ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, ilikuja baada ya kuibuka kwa malumbano katika Bunge hilo na kuishia kwa matusi na kashfa  kwa viongozi wakuu wa nchi pamoja na waasisi wa Taifa la Tanzania.
Naye Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, aliilenga moja kwa moja Chadema inayoongoza Ukawa kuwa inahusika na hatua ya kukashifu waasisi.
Alisema hayo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kata ya Majimoto, wilayani Mlele, mkoani Katavi, wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana ya kuimarisha chama hicho.
Nape alidai baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu kutoka Chadema, walifanya mkutano wa siri na kukubaliana ili wafanikiwe kuwarubuni Watanzania kuhusu Muungano, wamtukane Mwalimu Nyerere.
"Nilipopata taarifa hizi sikuamini, lakini Aprili 12, mwaka huu, Lissu alisimama bungeni bila aibu na kudai kuwa eti Nyerere amezoea vya kunyonga vya kuchinja hawezi, hii ni aibu yaani Lissu huyu amefikia hatua ya kumtukana mtu aliyemfikisha hapo alipo? Alihoji.
Alisema katika kauli ya Lissu bungeni, pia alidai kuwa Nyerere hakuipenda Tanzania ambapo alizoea kuishi kwa uongo na utapeli.
"Hivi kweli tunathubutu kumzungumzia uongo kiongozi kama huyu ambaye mpaka sasa hajafuta historia ya kuwa mzalendo namba moja hapa nchini?" Alihoji.
Kwa mujibu wa madai ya Nape, katika kikao hicho alikuwepo Mjumbe Vincent Nyerere, ambaye alipoona wenzake wanalenga kuvunja Muungano kwa kumtumia Mwalimu Nyerere, aliamua kutoka katika kikao hicho.
Muda mfupi baada ya kupata taarifa ya kuwasili kwa Hati ya Muungano bungeni, na kwamba jamii inahoji uhalali wao wa kuwakashifu waasisi wa Taifa, Mjumbe Julius Mtatiro, alipewa nafasi ya kuzungumza kuchangia taarifa za kamati zilizofikishwa bungeni, lakini alitoa nafasi hiyo kwa  mjumbe mwenzake, Profesa Ibrahim Lipumba.
Lipumba badala ya kujadili taarifa za kamati hizo,  alilaumu jinsi Bunge linavyoendesha mjadala na kudai unaendeshwa utadhani ni wa chama cha CUF, Chadema au Wapemba na kwamba Bunge limeacha kujadili Rasimu iliyoletwa na Rais kupitia Tume ya Mabadiliko ya Katiba na badala yake, kinachojadiliwa ni ubaguzi na kulifanya Bunge kama kikundi cha waasi cha Intarahamwe.
Ni Lipumba huyo huyo, wakati wa kuwasilisha taarifa za kamati na yeye kuzungumza katika nafasi ya wachache ya upendeleo ya kufafanua kuhusu hoja za wachache, alimshukuru Mwenyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, kwa kuendesha Bunge vizuri.
Profesa Lipumba alianza kwa kunukuu gazeti, tofauti na taarifa za Kamati za Bunge ili kujenga hoja ya kufungasha virago, na kusema  kama Serikali ilikuwa inajua kwamba hakuna haja ya kujadili Rasimu hiyo, kulikuwa na sababu gani ya kupoteza mabilioni ya fedha kwa Tume hiyo kukusanya maoni na kukarabati jengo la Bunge huku ikijua wazi kuwa, kinachotakiwa kwa namna yoyote ile ni serikali mbili na si serikali tatu kama mapendekezo ya Rasimu inavyoeleza.
Huku akijua kuwa wajumbe wa Ukawa wameshachukua posho za mpaka Aprili 30 mwaka huu, alishawishi wajumbe wa Ukawa kutoka nje  ya ukumbi wa Bunge, kwa madai ya kutoridhika na namna Bunge linavyoendeshwa.
Baada ya kutoa hoja zake kutoka katika gazeti, Lipumba alisema Ukawa hawawezi kuendelea kukaa ndani ya Ukumbi wa Bunge na aliongoza wajumbe hao kutoka nje ya ukumbi huo huku wakiimba na kupiga makofi na kelele kwamba Serikali ya CCM ni sawa na jeshi la waasi la Intarahamwe.
Nje ya ukumbi wa Bunge, wajumbe hao baadhi wakiwa wameshikana mikono, waliongozwa na viongozi wao wa juu akiwemo Mwenyekiti wa Ukawa na Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila na Lipumba mwenyewe, walisikika wakisema wamechoka kutukanwa, kuonewa na kubaguliwa na saa ya ukombozi ni sasa.
"Tumechoka kubaguliwa na hatutarudi kamwe humo ndani, tunabaguliwa kwa misingi ya rangi, vyama vya siasa, Upemba, huyu mwarabu na kukataa kujadili rasimu iliyotumia mabilioni ya fedha za walipa kodi, si sahihi, hatukubali tena na sasa tutaishitaki serikali kwa wananchi, hao ndio wataamua si sisi," walisikika wajumbe hao wakisema kwa nyakati tofauti, huku wakijua wameshachukua posho za mpaka Aprili 30 mwaka huu.

No comments: