UJENZI WA MTANDAO WA MAWASILIANO WA SERIKALI WAANZA

Serikali imesaini mikataba miwili na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) pamoja na Soft Net kwa ajili ya ujenzi wa mtandao wa mawasiliano wa serikali utakaohusisha taasisi 72.
Akizungumza jana Dar es Salaam kabla ya kusaini mikataba hiyo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, George Yambesi alisema lengo la mradi huo ni kupanua wigo wa upatikanaji wa taarifa muhimu katika kila ngazi ya serikali.
Alisema kampuni hizo zimeshinda zabuni na ndizo zitajenga  mtandao huo. TTCL ni wajenzi wataosambaza nyaya zitakazounganisha taasisi hizo na Kampuni ya Soft net watatoa vifaa vitakavyounganisha mtandao huo wa serikali.
Alisema mradi huo utahusisha taasisi 72 ambazo ni wizara zote, idara 16 zinazojitegemea, na wakala za serikali 30.
Taasisi zilizobaki zikiwemo Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaunganishwa kutokana na upatikanaji wa fedha.
Mradi huo unaogharimu dola za Marekani milioni 1.8, unalenga kuweka mtandao mmoja wa mawasiliano serikalini katika taasisi zote,  kuipa serikali na taasisi zake mawasiliano ya sauti, data, nyaraka na picha.
Unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na unatarajia kukamilika ndani ya miezi 20.

No comments: