UJENZI WA HOTELI ZAIDI HIFADHI YA NGORONGORO SASA BASI

Rais Jakaya Kikwete amesema Serikali haitaruhusu ujenzi wa hoteli nyingine katika Hifadhi ya Mamlaka ya Ngorongoro, akisisitiza kuwa zile 50 zilizopo sasa zimetosha.
"Kwa wale wawekezaji waliokuwa na ndoto za kujenga hoteli au loji za kitalii katika uwanda wa Ngorongoro hivi sasa wafikirie zaidi kuzijenga katika mji wa Karatu," alisema Rais Kikwete wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Karatu, Ngorongoro na Mto-wa-Mbu waliokusanyika kumsikiliza katika viwanja vya Mazingira Bora, mjini hapa.
Eneo la Ngorongoro, ambalo ndiyo kivutio maarufu zaidi nchini kwa kupata watalii zaidi ya 500,000 kila mwaka, ni moja ya maeneo rasmi ya Urithi wa Dunia, yaliyoteuliwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na masuala ya Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco).
Rais Kikwete ambaye alifanya ziara ya siku moja mjini Karatu baada ya mapumziko ya Pasaka katika hifadhi ya Ngorongoro, amebainisha kuwa hivi sasa ni wakati muafaka  wa kuinua mji wa Karatu kuwa eneo maalumu la kupumzikia watalii wakiwa njiani kwenda au kutoka kwenye hifadhi za Ngorongoro, Serengeti na Ziwa Manyara.
"Tunataka wageni watembelee Serengeti na Ngorongoro ili kujionea vivutio mbalimbali, hususani wanyamapori, lakini ni vizuri wawe wanafikia katika hoteli zitakazojengwa katika mji wa Karatu," alisema Rais Kikwete.
Takribani watalii 79,000 hulala katika hoteli zilizomo  ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Kiongozi huyo wa nchi pia ameelezea mipango ya serikali yake kupanua uwanja mdogo wa ndege wa Ziwa Manyara, ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu yake, kuwezesha ndege  zaidi za kitalii kutua wakati wote, katika jitihada za kuinua sekta ya utalii katika ukanda huu wa kaskazini.

No comments: