TUME YAUNDWA KUCHUNGUZA MAUAJI YA MPAKANI

Tume ya watu 18 iliyoundwa kuwabaini na kuwakamata watu waliohusika na mauaji ya watu watano katika mapigano ya wakulima na wafugaji yaliyotokea mpakani mwa mikoa hiyo miwili imetakiwa kuharakisha kazi yake.
Wajumbe wa tume hiyo ni pamoja na wenyeviti wa kamati za ulinzi na usalama wakiwemo  Wakuu  wa mkoa wa Shinyanga, Ally Rufunga na mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa  Chama cha Mapinduzi(CCM)  mkoani Shinyanga, Khamis Mgeja kwenye kikao cha ndani cha CCM kilichofanyika wilayani Kishapu wakati wa ziara ya Mkuu wa mkoa, Rufunga wilayani humo.
Kauli ya mwenyekiti huyo ilitokana na taarifa ya mauaji iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Wilson Nkhambaku.
Nkhambaku alisema kuwa mapigano hayo yalitokea Machi 29 mwaka huu katika kijiji cha Magogo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga mpakani na wilaya ya Igunga mkoani Tabora.
"Migogoro ya ardhi hapa nchini inapaswa kukemewa ikiwa inavunja amani ya nchi na hakuna kitu kibaya kama vita vya wenyewe kwa wenyewe ikiwa asilimia kubwa ya mapigano hayo watu hujuana udhaifu  wao na hivyo kulitia hasara taifa kwa kupoteza nguvu kazi na kupunguza pato la taifa," alisema Mgeja .
Hata hivyo  alisema kuwa moja ya utekelezaji wa ilani ya CCM ni kuhakikisha watanzania wote wanaishi kwa mshikamano, amani, upendo na chama hicho hakitakubali mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi na kuitaka tume hiyo ya watu 18 ya mikoa yote miwili Tabora na Shinyanga kuhakikisha watu hao wanakamatwa.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo ya Kishapu  alisema  tume hiyo ya pande zote mbili zilikutana na kujadili walipofikia na kudai kuwa bado wanaendelea na uchunguzi huku akiwataja watu waliouawa katika mapigano hayo kuwa ni Peter Korongo Masolwa(72) Chawalwa Duke(50) Diblo Kingu(50) Mohamed msengi(40) na Kende Doma(70).
Nkhambaku pia alimtaja mtu aliyejeruhiwa katika mapigano hayo kuwa ni Gilijisiji Gilawida ambaye alijeruhiwa kwa kuchomwa mkuki na kudai kuwa hali yake inaendelea vizuri .
Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la polisi mkoani Shinyanga,  Evarist Mangala alisema mpaka hivi sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na mauaji ya watu hao watano yaliyotokea katika mapigano ya kugombea ardhi ikiwemo mto Manonga  baina ya wafugaji wa Kishapu Mkoani Shinyanga  na wakulima wa Igunga Mkoani Tabora.

No comments: