TUCTA WAMFAGILIA JK, MGENI RASMI MEI MOSI

Rais Jakaya Kikwete anatarajia kuwa mgeni rasmi katika sherehe za wafanyakazi, Mei Mosi zitakazofanyika mapema wiki ijayo huku wafanyakazi wakieleza imani waliyonayo kwa Rais huyo katika kushughulikia matatizo yao na kuongeza kuwa, wanaamini dosari zinazojitokeza zinasababishwa na watendaji wake.
Kutokana na hilo, wamedhamiria kumsaidia Rais katika kuwaondoa watendaji hao katika nyadhifa zao kwa kuwa ndio wanaofanya siku zote kuonekana wafanyakazi wana matatizo na serikali.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Hezron Kaaya wakati alipokutana na wanahabari jana kuzungumzia maadhimisho ya Sikukuu ya Mei Mosi mwaka huu yatakayofanyika kitaifa mkoani Dar es Salaam.
Kaaya alisema walipokutana na Rais Kikwete Aprili 17 mwaka huu walibaini kuwa Rais anakerwa na kutokuwepo utekelezaji wa madai ya wafanyakazi kutokana na kuwabana watendaji ambao walishindwa kujieleza.
Alisema baada ya sherehe za Mei Mosi, Mei 5 mwaka huu watakaa kikao cha mwisho cha mashauriano  na baada ya hapo watachukua hatua za kushinikiza watendaji hao kuondoka kwani hawatimizi wajibu wao.
“Katika kikao chetu na Rais Kikwete alishangaa kuwa suala la kuwa kuna mambo bado yamelala licha ya kuwa yameshafanyiwa kazi.
Kuna suala la ukokotoaji kwa mifuko yote ya jamii kutofanyiwa kazi licha ya kuwa tayari wamefanya tathmini, mshauri kaishafanyia kazi, lakini bado linasuasua,” alisema.
Alisema Rais pia alishangaa kwamba suala la kodi linaendelea kuwalemea wafanyakazi wachache walioko katika sekta rasmi na kuacha wengine wakiwa hawalipi kodi kwani nguvukazi ya nchi ni zaidi ya watu milioni 21, lakini wanaotozwa kodi ni milioni tatu pekee.
Alibainisha wazi kuwa baada ya majadiliano ya muda mrefu, Rais aliwaagiza Waziri wa Fedha na Waziri wa Kazi na Ajira kufanyia kazi madai yote ili aweze kueleza wafanyakazi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi.
maadhimisho ya Mei Mosi mwaka huu, Kaaya alisema kwa mwaka huu maadhimisho yake yatakuwa tofauti na miaka mingine ambapo yatakuwa na wiki ya Wafanyakazi kuanzia Aprili 27 hadi 30, mwaka huu na kilele chake kufanyika katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Alisema katika siku hiyo, maandamano yataanzia Mnazi Mmoja na kuishia katika viwanja hivyo yakipokewa na Rais Kikwete ambaye atazungumza na wafanyakazi.
Alisema wiki hiyo itazinduliwa na Makamu wa Rais, Mohamed Gharib Bilal Aprili 28 mwaka huu ikiwa sambamba na Siku ya Afya Duniani inayoadhimishwa, siku hiyo ikiwa ni pamoja na maonesho yatakayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

No comments: