TTCL YATOA MISAADA VITUO VYA WATOTO YATIMA

Wakati Wakristo  duniani  kote wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka, Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) imetumia fursa hiyo kutoa msaada wa vyakula kwa vituo vitatu vya watoto yatima
Akikabidhi msaada huo, Mkuu wa Biashara Mkoa wa Dar es Salaam wa TTCL, Karim Bablia alisema msaada huo ulilenga kuvisaidia vituo hivyo vya kulelea watoto yatima vya jijini Dar es Salaam ili nao waweze kusherehekea vyema Sikukuu hiyo ya Pasaka.
“Kampuni yetu imeamua kusherehekea pamoja na watoto hawa ambao pia ni sehemu ya jamii yetu,” alisema Bablia.
Alivitaja vituo vilivyopatiwa msaada huo kuwa ni pamoja na Hananasifu cha Mkwajuni Kinondoni, Yatima Group cha Chamazi Mbagala na Chakuwama cha Sinza Mori.
Alisema msaada huo ni  pamoja na kilo 450 za mchele, maharage kilo 300, unga kilo 750, katoni 100 za maji ya kunywa, lita 120 za mafuta ya kula na sabuni katoni 15 ambapo vituo hivyo vyote vitagawiwa.
Alisema msaada huo ni sehemu ya ushirikiano mzuri kati ya TTCL na wateja wake hivyo kuwapatia watoto yatima ni sawa na kurudisha fadhila kwa wateja wao kutokana na ushirikiano wao.
“Tunatambua kuwa kulea na kutunza watoto yatima ni wito mkubwa kwa watu au vituo vilivyojitolea kufanya hivyo,” alisema Bablia.
Mkurugenzi Msaidizi wa Yatima Group, Haruna Mtandika alisema kituo chao kina watoto 179 ambao wanasaidiwa kwa kulelewa na kupatiwa mahitaji mbalimbali ya kibinadamu.
“Tunaishukuru Kampuni yetu ya TTCL kwa kutupatia msaada wa vyakula, hii itasaidia watoto wetu kusherekea vyema Sikukuu hii ya Pasaka,” alisema.
Alisema kituo chao kimejitolea kulea watoto yatima ambao walikuwa wanaishi katika mazingira magumu sana ili waweze kupata huduma za msingi ili baadaye waje kuwa watu wanaoweza kujitegemea.
Naye Katibu  Mtendaji wa Chakuwama, Hassan Hamis alisema anashukuru msaada huo kwa vile watoto wake nao watafurahia Sikukuu ya Pasaka.
“Kituo chetu kina watoto 90 na kinajitahidi kadiri ya uwezo wake katika kulea watoto hao yatima lakini kinakabiliwa na changamoto mbalimbali,” alisema Hamis.

No comments: