TBS, ZBS WAZUNGUMZA KUMPATA WA KUWAKILISHA ISO

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema lipo katika mazungumzo na Shirika la Viwango la Zanzibar (ZBS), kukubaliana nini kifanyike kupata uwakilishi mmoja kwenye Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO).
Kwa mujibu wa TBS, ISO inatambua uwakilishi wa shirika moja la viwango kutoka katika nchi mwanachama, lakini Tanzania inayotambuliwa kama nchi ina mashirika mawili, hivyo kuleta ugumu kwenye shirika hilo kuhusu utambuzi.
Akizungumza Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi wa viwango wa shirika hilo, Leandri Kinabo alisema, kutokana na sharti hilo, Tanzania haina budi kutaja uwakilishi mmoja.
“Kwa sababu Tanzania Bara tuna shirika letu la viwango yaani TBS na Zanzibar wana la kwao yaani ZBS, tunapaswa kukubaliana na kutoka na jibu moja la shirika lipi litambuliwe na ISO kama mwakilishi katika nchi au nini kifanyike kutuwakilisha wote.
“Tunapotajwa kuwa ni nchi moja ni lazima tuwakilishwe na shirika moja la viwango katika ngazi hiyo ya kimataifa. Kinyume na hapo, tunakuwa tumekiuka matakwa ya ISO, hivyo kujiweka katika hatihati ya kutotambuliwa,” alisema.
Kinabo ambaye alizungumza kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko alisema, tayari TBS ilikwisha anza mazungumzo na ZBS na kwamba, kutokana na umuhimu wa jambo lenyewe, bado wanaendelea kuzungumza kuhakikisha wanafikia uamuzi sahihi bila kupoteza wakati.

No comments: