TAKUKURU WAITWA KUCHUNGUZA TANESCO, EWURA, TPDC, MADINI

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ametaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuchunguza wafanyakazi wa wizara hiyo na mashirika yake wanaotuhumiwa kwa rushwa. 
Ametaka Takukuru na vyombo vya dola kwa ujumla, kufanya uchunguzi kwenye Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) na Idara ya Madini.
Waziri Muhongo, alitoa agizo hilo kupitia hotuba yake kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo katika mkutano wake wa kwanza wa 2013/2014 wa siku mbili unaofanyika mkoani Morogoro.
Kwa upande wa Idara ya Madini, Waziri alisema anawasiliana kiofisi na Takukuru ili watendaji wake wafike Makao Makuu wa Idara hiyo kuchunguza watendaji na wafanyakazi.
Sababu ya kuanza na Idara hiyo, Profesa Muhongo alisema ni     kutoridhishwa na hatua ya viongozi kushindwa kufuta leseni za  vitalu vya watu waliohodhi miaka mingi bila kuendelezwa kinyume na Sheria ya Madini.
Licha ya kusema sekta ya madini inakabiliwa na matatizo ya ucheleweshaji wa utoaji wa leseni na kushindwa kuwafutia wachimbaji ambao wamepewa vitalu vikubwa vya ardhi, imeonekana vinamilikiwa na wafanyakazi wake na vitatolewa kwa wachimbaji kwa njia ya rushwa.
“Inaonekana kusuasua kwa kushughulikia kutoa leseni kwa wachimbaji wanaohitaji na kuwafutia wale wanaoshindwa kuendeleza vitalu hivyo kunatia shaka, inaonekana vitalu hivyo ni vya baadhi ya wafanyakazi wa sekta ya madini ambao wametumia majina tofauti tofauti kuvimiliki. 
“Kutokana na hali hii kwamba kuna uwezekano vitalu vingi vinashikiliwa na wafanyakazi wa Idara ya Madini, kuanzia  Julai Mosi mwaka huu, Kamishna wa Madini asipovifuta kwa mujibu wa Sheria ya Madini  nitaialika Takukuru waingie ili kufanya uchunguzi na  watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
“Tukiangalia tutagundua wafanyakazi wengi wa Idara ya Madini wamejichukulia vitalu vingi vya madini na kuwatafuta watu kwa kuwauzia kwa njia isiyo halali na jambo hili kimaadili na kisheria si sahihi. Takukuru itafanya kazi yake,” alisisitiza.
Aidha alitaka baraza hilo kupunguza mlolongo wa kupatikana kwa leseni za uchimbaji.
“Ni vyema kikao hiki cha Baraza kitoe majawabu kuhusu kuondoa urasimu huu, ili kuwezesha mwombaji apate leseni ndani ya siku mbili kutoka saba ama wiki mbili kutoka mwezi mmoja na kuwezesha wadau na wawekezaji kuvutiwa,” alisema Waziri Muhongo.
Hata hivyo alitaka Idara hiyo iboreshe mfumo mpya utakaoanza kutumiwa kuanzia Julai mosi mwaka huu kwa njia ya mtandao na  kutoa majawabu ya masuala yote muhimu katika utendaji wa sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo alisema, Serikali imepanga kutoa Sh bilioni 2.3 za mikopo kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini, lengo likiwa kuwaendeleza ili watoe mchango mkubwa  kwa pato la Taifa na kuziba pengo la wawekezaji wakubwa. Awali, Kamishna wa Madini, Paul Masanja, alisema wameshaanza kufanya uchambuzi wa maombi ya leseni na vitalu visivyoendelezwa kwa lengo la kuchukua hatua zinazostahili.
Alisema hadi Julai Mosi mwaka huu, leseni zisizoendelezwa zitafutwa sambamba na kutumia mfumo wa mtandao kuomba na kutoa leseni.
Kwa mujibu wa Kamishina wa Madini, leseni zilizofutwa ni 184, zilizositishwa ni 80 na 150 zipo katika ufuatiliaji ili zifutwe rasmi.

No comments: