SUMATRA YAONYA UPANDISHAJI HOLELA WA NAULI

Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imeonya wanaopandisha  kiholela nauli za mabasi wakati maandalizi ya sikukuu ya Pasaka.
Ofisa Mfawidhi wa Sumatra Kanda ya Mashariki, Conrad Shiyo aliliambia gazeti hili jana na kuongeza kuwa wanakusudia kufanya ukaguzi mkali kuwabaini watakaohusika na suala hilo.
"Kumekuwa na tabia ya baadhi ya wenye mabasi kupandisha nauli bila utaratibu nyakati za sikukuu kwa ili kupata faida,  tumejipanga ‘kuwakomesha wahusika’ wa matendo hayo," alisema.
Alisema tabia hiyo inayofanywa na wenye mabasi hayo hususani mawakala mara nyingine imekuwa ikisababisha usumbufu kwa abiria na kusababisha baadhi yao kushindwa kusafiri kutokana na nauli hizo kuwa juu tofauti na zile zilizozoeleka.
Aidha alisema tayari Sumatra imeweka maofisa wake katika vituo vyote vya mabasi nchini na hasa katika kituo Kikuu cha mabasi cha Ubungo, ili kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo na hivyo kutoa fursa kwa wasafiri wote kuepukana  na usumbufu wakati wa kusafiri.

No comments: