SITTA APONGEZA WAJUMBE KWA KUFIKA BUNGENI KWA WAKATI

Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amewapongeza wajumbe wa Bunge kwa kufika kwa wakati katika vikao na kusisitiza kuwa kazi walio nayo ya kutunga Katiba si kazi ya mchezo kwani inahitaji busara, uvumilivu na ukomavu mkubwa wa kisiasa.
Sitta amesema anaamini kuwa Mungu anaipenda sana nchi ya Tanzania na kutokana na ukweli huo, Katiba mpya inayolinda maslahi ya Taifa na watu wake, itapatikana.
Aliyasema hayo jana bungeni, mjini hapa mara baada ya kuanza kwa kikao cha Bunge hilo baada ya mapumziko ya sikukuu ya Pasaka yaliyoanza Ijumaa Kuu hadi juzi Jumatatu.
Mwenyekiti huyo alisema, hivi sasa wajumbe wengi wanafika katika vikao kwa wakati na Bunge linaanza kwa muda uliowekwa hivyo hata hatua ya kutunga Katiba, itawezekana na Katiba mpya ya Tanzania, itapatikana.
Nae mjumbe wa Bunge hilo, Hamis Damumbaya alisema kunahitajika maridhiano katika kutunga Katiba.
Alisema ni vyema wanasiasa wakajenga urafiki katika mchakato huo wa uundaji wa katiba kwani ni muhimu kuelewana katika masuala kitaifa.
Damumbaya alisema hakuna sababu ya vyama vya siasa kukimbia kwa wananchi na kuanza kulalamika badala yake wanapaswa kutumia maridhiano kutafuta maridhiano.
"Wajumbe kukimbia Bunge ni jambo la aibu kwa Watanzania, Taifa hili linasifa yake ndani na nje ya nchi hivyo ni muhimu kuilinda," alisema Damumbaya.

No comments: