SERIKALI KUDHIBITI WASICHANA KWENDA CHINA

Serikali imesema iko katika mikakati kuhakikisha inadhibiti vitendo vya wasichana kwenda China bila sababu maalumu ikiwa ni njia ya kudhibiti vitendo vya watoto wa kike kujihusisha kwa biashara ya ukahaba nchini humo.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani pamoja na Ubalozi wa China nchini, zimeamua kuchukua hatua hiyo.
Sanjari na kulenga kuzuia wanaokwenda nchini humo bila shughuli zinazoeleweka, mkakati huo pia utashughulikia walioko nchini humo wakifanyishwa vitendo hivyo, warejee nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa  Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ally alisema hayo hivi karibuni akizungumza na mwandishi.
Alikuwa anazungumza na mwandishi juu ya hatua za serikali kukabili wimbi la wasichana wa kitanzania  wanaodaiwa kufanya bishara ya ukahaba China, kama ilivyoelezwa hivi karibuni na Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Katika mikakati inayofanywa na nchi hizi mbili (Tanzania na China), wanataka kuhakikisha hatua stahili zinachukuliwa  kwa wanaohusika na vitendo hivyo pamoja na waliowapeleka hatimaye kudhibiti mtu yeyote kwenda China  kiholela.
“Kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani, Ubalozi wa China na serikali yake pamoja na vyombo husika, tunafanya juhudi kuchukua hatua stahili ikiwa ni pamoja na kukabili  waliopo nchini humu na kuweka udhibiti isiwe rahisi kwenda,” alisema.
Wakati ikidaiwa kuwepo wasichana wanaofanyishwa vitendo hivyo vya ukahaba, vile vile yako malalamiko kwamba baadhi ya wananchi wanaopelekwa kufanya kazi Omani hunyang’anywa hati zao za kusafiria wanapofika nchini humo.
Hivi karibuni, Waziri Membe katika mkutano na waandishi wa habari, alieleza kuwapo kwa wasichana wadogo wanaopelekwa China na baadhi ya watu na kuwafanyisha biashara ya ukahaba.
Wakati wizara kwa kushirikiana na Serikali ya China wakidhamiria kudhibiti usafirishaji wa watoto hao wa kike kwenda kufanyishwa vitendo hivyo vya udhalilishaji, Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) wamewataka watu wanaotaka ajira nje ya nchi kupitia kwao  waweze kupata ajira zenye staha.
Akizungumza hivi karibuni na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msemaji wa  TaESA, Joseph Haule, alisema wakala hao walio chini ya Wizara ya Kazi na Ajira, wanahusika kuunganisha watafuta kazi na waajiri wenye fursa za kazi ndani na nje ya nchi.
Alisema kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi kwamba watu wanaopelekwa nje kufanya kazi wanafanyishwa kazi zinazowadhalilisha na kuwanyima haki zao.
Kwa mujibu wa msemaji huyo wa wakala, watu wengi ambao wamekuwa wakipita njia za panya, ndiyo hukumbwa na matatizo na yakishawapata, hulalamikia wakala wakati hawakuhusika katika kuwasafirisha.
“Sisi kabla hatujamsafirisha mtafuta kazi kwa mwajiri nje ya nchi lazima tuhakikishe tunawasiliana na balozi zetu zilizopo kwenye nchi hizo ili kuhakikisha ukweli wa kazi hiyo,” alisema Haule.
Pia alisema mpaka sasa mawakala hao wameshawatafutia kazi watafutakazi 2,614 na wote wako nje ya nchi na hakuna tatizo lililotokea kwa watu hao mpaka sasa.

No comments: