RC ATAKA DALADALA ZIENDE KWA WINGI UWANJA WA TAIFA LEO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik, ameitaka Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) na wamiliki wa magari ya abiria, kuelekeza Uwanja wa Uhuru, kurahisisha usafiri kwa wananchi watakaohudhuria maadhimisho ya Muungano.
Aidha, amewaomba radhi wananchi watakaohudhuria maadhimisho hayo, kwa upekuzi wakati wa kuingia uwanjani hapo, ambao lengo lake  ni  kulinda usalama.
Alisema hayo jana Dar es Salaam alipokuwa akizungumzia maadhimisho ya sherehe za Miaka 50 ya Muungano, zitakazofanyika kitaifa leo jijini hapa.
Alisema Muungano huo ni wa kujivunia kote duniani, kwani kuna nchi ziliwahi kujaribu kuungana, hazikufanikiwa, lakini nchi yetu imedumisha na kuuimarisha muungano.
"Tunatarajia kuwa na ugeni mkubwa  kwani marais karibu wote wa nchi jirani na Maziwa Makuu, watahudhuria katika hafla hiyo, makamu wa rais na mawaziri wakuu na wengine watakaohudhuria tunaomba muwapokee,’’ alisema.
Akizungumzia baadhi ya vitu vitakavyofanyika, Sadik alisema sherehe hizo zitapambwa na gwaride, halaiki, ngoma kutoka mikoa mbalimbali, zana na ndege za kivita, maandamano ya pikipiki na baiskeli.
Pia, alisema kwa wananchi wanaotimiza miaka 50 ifikapo leo, watahudhuria kushiriki katika sherehe hizo za Muungano.
Kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo, milango ya uwanja itafunguliwa saa 12 asubuhi, hivyo wananchi wote wanakaribishwa na wanatakiwa kuwahi mapema, pia kutakuwa na skrini kwa watakaokuwa nje.

No comments: