RAIS KIKWETE AZUIA VIGOGO KUTUMIA VIBAYA WODI YA MOYO

Rais Jakaya Kikwete ameuonya Uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), kutowafumbia macho na kuwaruhusu watu maarufu nchini, kutumia vibaya wodi za kisasa za Kituo kipya cha Upasuaji wa Moyo, Matibabu na Mafunzo cha hospitali hiyo.
Pia ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na Uongozi wa Muhimbili, kuandaa utaratibu na kuhakikisha kituo hicho kinafanya kazi kwa kujitegemea ili kiwe na ufanisi zaidi, kama ilivyo Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Mishipa ya Fahamu na Upasuaji wa Ubongo (MOI).
Alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo hicho, Dar es Salaam jana.
Rais Kikwete alisema Serikali haitavumilia kuona wodi hizo zikitumika vibaya kwa wagonjwa wasiokuwa wa moyo,  huku wagonjwa wa moyo wakikosa mahali pa kulazwa.
"Haitakuwa na maana ya kuwepo na kituo hiki, jiepusheni na ushawishi wa kugeuza wodi za kituo hiki kuwa cha watu maarufu na wenye fedha ambao si wagonjwa wa moyo," alisema.
Alisema kutokana na ubora wa wodi hizo, watu hao wana uwezo wa kulipa kiasi chochote cha fedha ilimradi walazwe, bila kujali wagonjwa wahusika wa moyo.
Kutokana na umuhimu wa kituo hicho nchini, hasa katika maendeleo ya sekta ya afya, Rais alitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na uongozi wa Muhimbili,  kuweka utaratibu wa kuhakikisha kinajitegemea  kama ilivyo MOI ili kijiendeshe kwa ufanisi.
"Kwa umuhimu wa kituo hiki, kikitegemea bajeti moja ya Muhimbili ndipo na chenyewe kipate mgawo, kuna uwezekano wa huduma muhimu kukosekana ni bora uwekwe utaratibu mapema, kwani Moi kama ingetegemea Muhimbili, ingekuwa katika hali mbaya kutokana na uhaba wa fedha," alisisitiza.
Pamoja na hayo, aliitaka Bohari ya Taifa  ya Dawa (MSD) kutambua umuhimu wa kituo hicho cha Moyo na kuhakikisha dawa na vifaa vya tiba vinapatikana wakati wote.
"Hapa napenda nisisitize kuwa Serikali haitakuwa tayari kusikia eti kituo hiki hakina dawa za kutosha wala vifaa, maana umuhimu wake kwa Watanzania hautakuwepo, MSD tambueni kituo hiki, ili lengo la kupambana na ugonjwa huu lifikiwe," alisema.
Alisema pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa takwimu zinazoonesha kuwa kila mwaka watu milioni 12 hufariki kwa ugonjwa wa moyo duniani, Tanzania kasi ya ongezeko la wagonjwa wa moyo ni kubwa, ambapo asilimia 26 ya wagonjwa hao, hufariki kila mwaka.
Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali ilitafuta msaada kwa Serikali ya China kupitia Rais Xi Jinping aliyekuwepo nchini hivi karibuni, ambapo alikubali China kuchangia ujenzi wa kituo hicho, kwa kutoa Sh bilioni 16.6 na Tanzania ilichangia Sh bilioni 10.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid, alisema  uwepo kwa kituo hicho,  utapunguza gharama za Serikali kusafirisha wagonjwa wa moyo nje ya nchi na kupunguza idadi kubwa ya vifo vya wagonjwa wa moyo, kutokana na ukosefu wa tiba hiyo nchini.
Alisema kituo hicho, ambacho tangu kianze mwaka jana kimeshafanya upasuaji wa wagonjwa 33, kitatoa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo, vipimo vya moyo kwa kutumia vifaa vya kisasa na uchunguzi wa mishipa ya damu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Muhimbili, Profesa Joseph Kuzilwa, alisema licha ya ukosefu wa kitengo maalumu cha tiba ya moyo nchini, hospitali hiyo ilishaanza kufanya upasuaji kwa wagonjwa wa moyo 362 tangu mwaka 2008.
"Lakini ni jambo la kujivunia kuwa sasa kuna kitengo maalumu cha tiba ya ugonjwa huu hatari, ambapo idadi ya wagonjwa itaongezeka kwa kuwa jengo hili lina vyumba vya upasuaji vitano, wodi 32 za uangalizi maalumu na vitanda 96 vya kulazia wagonjwa, pia kituo kina uwezo wa kuhudumia wagonjwa 400 kwa wiki," alisema.
Mjumbe Maalumu na Mwakilishi wa Rais wa China nchini, Xi Jinping ambaye pia ni Naibu Spika wa China, Chen Changzhi, alisema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya ishara ya urafiki na undugu baina ya China na Tanzania, ambao umedumu kwa   miaka 50 sasa.
Katika hafla hiyo, viongozi kadhaa waanzilishi wa ujenzi wa kituo hicho, walitunukiwa vyeti, akiwemo aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na aliyekuwa Mganga Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Deo Mtasiwa.

No comments: