POLISI YATANGAZA DAU MILIONI 10/- KUMNASA MLIPUAJI MABOMU

Baada ya mlipuko wa bomu kutokea juzi jijini Arusha, polisi imesihi wananchi kuchukua hadhari, hususan maeneo yenye mkusanyiko na kutoa taarifa  juu ya wanaowahisi mienendo yao si mizuri.
Aidha polisi imetangaza zawadi ya  Sh milioni 10 kwa mtu  atakayetoa taarifa juu ya wanaohusika katika kulipua  mabomu, ikiwa ni pamoja na waliolipua baa ya Arusha Night Park ya jijini hapa. 
Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu tukio hilo la Jumapili, saa 1:30 usiku eneo la Mianzini  kwenye baa hiyo inayomilikiwa na Joseph Kalugendo.
Alisema  wataalamu wa mabomu waligundua bomu lingine saa 6:00 usiku kwenye baa iliyo karibu na baa hiyo likiwa ndani ya begi dogo.Uchunguzi wa awali umebaini bomu hilo ni kifaa cha mlipuko wa kutengenezwa kienyeji.
Alisisitiza hadi sasa, hawajakamata mtu yeyote kuhusu tukio hilo huku uchunguzi ukiwa unaendelea.
Alisema majeruhi waliobaki wadini ni  wanane na wengine wameruhusiwa. Walio wodini ni Evance Maleko, Evarist Richard, Petro James,  Christian Zakaria, Pius Shayo, Antelus Ishengoma, Sudi Ramadhani na Mariam Hans aliyepo  hospitali ya Selian.
Alitaka wamiliki wa kumbi za starehe, makanisani, msikitini na maeneo ya mikusanyiko  kujitahidi kuweka kifaa cha CCTV  kuwezesha kubaini wahalifu.
Kuhusu baa ya Night Park, alisema kwa kuwa  kulikuwa na CCTV upo uhakika mhusika atapatikana.  Tukio hilo  la kupigwa bomu ni la nne jijini hapa. La kwanza ni la Juni mwaka jana katika uwanja wa Soweto. Jingine ni Mei mwaka jana kwenye Kanisa Katoliki Parokia ya Olasiti lililoua watu wanne.
Pia la Shekhe Abdulkareem Jonjo ambaye ni Katibu wa Baraza Kuu la Waislam Tanzania (BAKWATA)  aliyejeruhiwa usoni kwa mlipuko wa bomu nyumbani kwake.

No comments: