POLISI MWANAMKE AIBA MTOTO, BABA MTOTO AHUSISHWA

Ofisa wa Jeshi la Polisi nchini, anashikiliwa na jeshi hilo mkoani Mbeya akituhumiwa kuiba mtoto mchanga mwenye umri wa siku saba.
Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kumtaja askari anayeshikiliwa kuwa ni Konstebo Prisca Kilwai mwenye namba WP 5367 ambaye eneo lake la kazi ni mkoa maalumu wa kipolisi wa Ilala katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.
Kamanda Msangi alisema WP Prisca alikamatwa juzi majira ya kati ya saa nne na saa tano asubuhi akiwa katika eneo la Meta jijini Mbeya alikokutwa akiwa na mtoto mchanga aliyemuiba.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda Msangi alisema mtoto mchanga aliyeibwa alifahamika kwa jina la Goodluck Saleh ambaye alizaliwa Aprili 6 mwaka huu huko mjini Kyela.
Aliwataja wazazi wa mtoto aliyeibwa kuwa ni Mboka Mwakibabile mkazi wa eneo la Njiapanda mjini Kyela ambaye ni mama wa mtoto na Saleh Issa Mwangosi mkazi wa Kasumulu ambaye ni baba wa mtoto huyo na ambaye pia anashikiliwa.
Alisema siku moja kabla ya siku ya tukio baba wa mtoto huyo alimjulisha mzazi mwenzie kuwa kuna shangazi yake ambaye kesho yake angefika nyumbani kwa mama wa mtoto kwa lengo la kumwona mtoto na pia aweze kumsindikiza kumpeleka mtoto huyo kliniki.
Alisema siku iliyofuata, yaani Aprili 6 mwaka huu majira ya kati ya saa sita na saa saba mchana shangazi huyo ambaye ni WP Prisca alifika nyumbani kwa mkwewe na baada ya kumsalimia mtoto huyo waliongozana wote wawili kukipeleka kichanga kliniki kama mzazi mwenza alivyokuwa amependekeza.
Alisema baada ya kufika kliniki walitakiwa kuwa na daftari na kwa kuwa hawakwenda nalo ikalazimu jitihada za kwenda dukani kununua daftari hilo zifanyike.
Kamanda huyo alisema shangazi huyo bandia alitoa kiasi cha Sh 2,000 na kumpa mama wa mtoto aliyekwenda moja kwa moja dukani huku akimwacha mwanaye kwa WP Prisca akijua kamwacha sehemu salama kwani alijua ni bibi yake, yaani shangazi wa mzazi mwenzie.
Ajabu ni kuwa mama huyo aliporudi na daftari lake hakumwona mkwewe wala mtoto, hali iliyolazimu aanze kuuliza watu waliokuwepo jirani ambao baadaye walimwambia kuwa walimwona mtu aliyemwachia mtoto akipanda pikipiki na kutokomea kusikojulikana.
"Baada ya hapo mama huyu akalazimika kutoa taarifa kituo kidogo cha polisi kilichopo pale Kyela na jitihada za kutafuta zilianza mara moja. Hatua ya kwanza ilikuwa ni kumkamata baba wa mtoto kwa kuwa moja kwa moja alionekana kuhusika katika njama za wizi huo," alisema.
Alisema baada ya kumkamata baba wa mtoto jitihada ziliendelea hadi juzi alipokamatwa maeneo ya Meta jijini Mbeya akiwa na kichanga hicho.
"Baada ya kumkamata na kupata tetesi kuwa ni ofisa wa jeshi tulianza kupeleleza na ndipo tukabaini ukweli na kuwa anatokea mkoa maalumu wa kipolisi wa Ilala Dar es Salaam."
Kamanda Msangi alisema kinachoendelea hivi sasa baada ya kumkamata ni mashitaka ya kijeshi ili kumfukuza kazi ikithibitika juu ya tuhuma zinazomkabili na hatimaye kufikishwa mahakamani.
Alisema pia uchunguzi wa awali unaonesha hakuna mahusiano yoyote ya undugu kati ya askari huyo na baba wa mtoto isipokuwa mahusiano yaliyopo ni ya kibiashara ambapo ilionekana kuna biashara ambazo wamekuwa wakifanya kwa kushirikiana.

No comments: