PINDA AONGOZA MAMIA KUAGA MWILI WA DC CHANG'A

Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameongoza viongozi kadhaa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuuaga mwili wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Moshi Chang'a ambaye aliyefariki Jumapili kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako alikuwa akipatiwa matibabu.
Shughuli ya kuuaga rasmi mwili wa marehemu Chang'a kwa wakazi wa mji wa Dar es Salaam ilifanyika jana nyumbani kwake Mbagala, Kibonde Maji, jijini Dar es Salaam. Mwili wake ulisafirishwa jana kwenda Kihesa, mkoani Iringa kwa maziko.
Akizungumza na waombolezaji hao kabla ya kutoa heshima za mwisho, Waziri Mkuu Pinda alisema amemfahamu Chang'a kwa muda mrefu kwa sababu sehemu kubwa ya utumishi wake ameifanya akiwa Serikalini.
 Pinda alitumia fursa hiyo kufikisha salamu za rambirambi kwa wafiwa kutoka kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye yuko safarini kikazi.
Katika salamu za Rais Kikwete, alisema kifo cha Chang'a kimepunguza safu ya uongozi na taifa kupoteza mhamasishaji hodari wa maendeleo.

No comments: