PINDA AAGIZA MADENI YA WALIMU YALIPWE KABLA YA JUNI 30

Waziri Mkuu Mizengo Pinda, ameiagiza Wizara ya Fedha kuhakikisha  madeni ya walimu yamelipwa hadi kufikia Juni 30 mwaka huu, ili Serikali isiingie na madeni katika Bajeti ijayo.
Mbali na madeni ya walimu, Pinda alitaka pia madeni ya makandarasi,  pembejeo na mengineo, kulipwa ifikapo Juni 30 kutokana na madeni kuchangia kutotekelezwa vizuri kwa Bajeti ya mwaka huu.
Pinda alisema hayo jana wakati wa kikao cha wabunge cha kupokea taarifa ya mfumo wa Bajeti kwa mwaka 2014/2015  na kutaka Wizara hiyo, kuhakikisha inalipa madeni haraka.
Alisema Bajeti iliyopita, ilikumbana na changamoto nyingi, lakini katika Bajeti ya sasa, wamejipanga kuhakikisha changamoto hizo hazijirudii na inatekelezeka, kama ilivyopangwa na kutaka wabunge kupitia maelezo ya Waziri na kuyachambua kwa makini.
“Bado Bajeti inategemea misaada kutoka nje na mikopo mpaka nchi itakapokuwa na uwezo wa kujitegemea kwani kila mwaka inapungua taratibu hasa baada ya gesi toka Mtwara kufika jijini Dar es Salaam na kuwa na umeme wa uhakika na viwanda vingi kuongeza uzalishaji,” alisema Pinda.
Pinda alisema  katika kukabiliana na tatizo la mapato yasiyokuwa na kodi na katika Serikali za Mitaa kutofikiwa malengo wameunda timu maalum ya kufanyia utafiti suala hilo kwa nini hayafikii malengo na kupitia kila halmashauri kila baada ya miezi mitatu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mahusiano na Uratibu, Stephen Wasira alisema thamani ya wazi ya utekelezaji wa miradi ya Matokeo Makubwa Sasa, imeonesha mafanikio mazuri na kukubalika kwa utaratibu huo mpya.
Wasira alisema hayo wakati akiwasilisha Rasimu ya mpango wa maendeleo wa taifa kwa mwaka 2014/2015 katika Bunge lililokaa kama kamati.
Alisema katika kilimo, wametoa mafunzo ya skimu za umwagiliaji kwa maofisa ugani 95 na wakulima 95.
Alisema katika nishati, wateja wapya 138,931 wameunganishiwa umeme dhidi ya lengo la kuunganisha wateja 150,000 kwa mwaka 2013/2014 na kupunguza upotevu wa umeme kutoka asilimia 21 hadi 19.

No comments: