OLUOCH AOMBA WANANCHI WAULIZWE KUHUSU MUUNGANO

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Ezekiah Oluoch  amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua ya kuwasilisha muswada katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hati ya dharura ili kuifanyia marekebisho Sheria ya Marekebisho ya Katiba.
Alisema lengo la kurekebisha sheria hiyo ni ili kumpa mamlaka Rais kuahirisha Bunge Maalum kwa muda wa miezi sita ili kuruhusu kura ya maoni juu ya aina ya muungano wanaotaka wananchi yaani wa serikali mbili au tatu.
Pia alimtaka Rais kufanya marekebisho juu ya Ibara ya 74 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hati ya dharura ili kuweka Tume huru ya uchaguzi itakayosimamia uchaguzi wa mwaka 2015 na kura ya maoni.
"Ndani ya miezi hiyo sita ikiwa wananchi watachagua serikali mbili tume ya Jaji Warioba italazimika kuitwa tena na kuandaa rasimu ya serikali mbili na endapo wananchi watakubaliana na mapendekezo ya serikali tatu basi wajumbe watarudi kwa ajili ya kujadili yaliyomo kwenye rasimu ya sasa," alisema.
Olouch akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma.
Sambamba na hilo, alisema kitendo cha Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba (UKAWA) kutoka ndani ya Bunge hilo kimeelezwa kuchangiwa na Mwenyekiti wa Bunge hilo Samuel Sitta na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kutozingatia kanuni za Bunge hilo.
Oluoch alisema aliwasilisha hoja kwa Mwenyekiti wa Bunge hilo mnamo Februari 3, mwaka huu juu ya mwenendo wa Bunge hilo kutokana na kile alichodai aliziona dalili za kutokea matatizo ikiwemo mipasho pamoja na lugha zisizo za staha kwa baadhi ya wajumbe.
Kwa mujibu wa Oluoch, matatizo hayo yalianza tangu wakiwa wanatengeneza kanuni za Bunge hilo.
"Baada ya kukamilika kwa kanuni za Bunge Maalumu kuna vipengele viwili ambavyo havikutumiwa vizuri na Mwenyekiti wa Bunge hilo, kwanza ni matumizi ya lugha zisizo na staha kwani Mwenyekiti aliruhusu wajumbe kuchangia hoja kwa kupeana mipasho kulingana na aina ya hoja bila kujali hoja iliyoko mezani.
"Kanuni inamzuia mjumbe kuongelea hoja ambayo haikuwa mezani kwa majadiliano, lakini katika Bunge hili wajumbe wanachangia kwa kutoka nje ya hoja ilimradi kuudhi upande mwingine na Mwenyekiti hachukui hatua," alisema.
Oluoch anayewakilisha walimu katika kundi la 201 alisema wajumbe wenye kura turufu kuhusu aina ya muungano ni Wazanzibari kuliko wajumbe wa Tanzania Bara, hali aliyodai inatokana na ukweli kwamba zinahitajika theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar hivyo ni rahisi kuwashawishi wajumbe wa Zanzibar wakiwa ndani ya Bunge kuliko kutaka kuwaunganisha wakiwa nje ya Bunge hilo.

No comments: