NYUMBA ZA WENYE KIPATO CHA JUU KUJENGWA MSASANI

Liu Yupeng (kulia) akiongea na waandishi wa habari, Dar es Salaam jana.
Eneo linalotazamana na fukwe za Msasani jijini Dar es Salaam linatarajiwa kujengwa nyumba 98 za kiwango bora zikiwalenga wananchi wa kipato cha juu  na kati.
Mradi wa ujenzi wa nyumba hizo unajulikana kama 'HUAFU' na utatekelezwa na Kampuni ya DongXing International Real Estate Limited ambao utatoa huduma ya nyumba bora na ya kiwango cha juu.
Meneja Msaidizi wa kampuni hiyo, Liu Yupeng alisema hayo jana Dar es Salaam.
Alisema mradi  huo unatekelezwa katika eneo lenye mita za ujazo 20,220 na vyumba vyote ni vya kiwango cha juu vikitazama baharini.
"Kampuni hii iliingia nchini na kuendesha shughuli zake miaka miwili iliyopita mara baada ya kupata usajili rasmi wa kuendesha shughuli zake nchini, ilielekeza nguvu zake katika kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba ili kuweza kupunguza tatizo la nyumba bora za kuishi kwa wananchi wengi," alisema Yupeng.
Alisema pamoja na kuchangia mapato ya serikali kwa kiasi kikubwa, utekelezaji wa mradi huu utakuwa chanzo kikubwa sana cha ajira kwa vijana wengi wa kitanzania, hivyo kuweza kuchangia kipato chao kwa ajili ya kuendeleza maisha yao.
Aidha aliipongeza serikali kwa ushirikiano wake wa dhati na wawekezaji hasa katika suala la sera za kodi ambazo zimekuwa zikisaidia sana uendelezaji wa sekta ya nyumba na makazi.

No comments: