MWANDISHI WA HABARI MKONGWE AFARIKI DUNIA

Mwandishi wa Habari Mkongwe, Maurus John Sichalwe amefariki dunia asubuhi ya kuamkia jana  nyumbani kwake Mwananyamala Kanisani akiwa na umri wa miaka 83.
Taarifa iliyotolewa na mtoto wa marehemu, Benedict Sichalwe ilieleza kuwa  Sichalwe  alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tumbo.
Katika uhai wake,  Sichalwe alianza kufanya kazi mwaka 1952 katika magazeti ya Nationalist na kufanya kazi ndani na nje ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na All Radio India mjini New Delhi, India miaka ya 1960 mwanzoni.
Pia, Sichalwe alifanya kazi zaidi ya miaka 20 katika kampuni za magazeti ya Standard na Nation, alikofikia nafasi ya cheo cha Naibu Mhariri Mtendaji wa gazeti la Taifa Leo. Baada ya kurejea nchini Tanzania Desemba 1983, alifanya kazi katika Kampuni ya Magazeti ya CCM ya Uhuru na Mzalendo kwa miaka nane kutoka 1984 – 1992.
Mwaka 1992  alihamia Kampuni ya Business Times katika maandalizi ya kuanzishwa kwa gazeti la kwanza la kila siku binafsi kwa lugha ya Kiswahili la Majira. Lakini, alikaa kwa muda mfupi hapo, kabla ya kuhamia katika gazeti la kwanza la michezo la Dimba, ambalo lilikuwa linamilikiwa na Kampuni ya Habari Corporation Limited.
Alikuwa Msanifu habari wa gazeti la Dimba na  alidumu katika kampuni hiyo, iliyoanza kuchapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, Bingwa na The African. Alifanya kazi na kampuni hiyo kwa zaidi ya miaka 15 hadi  alipostaafu kazi katika fani ya habari, akiwa mmoja kati ya waandishi wa habari waliodumu kwenye fani kwa zaidi ya miaka 50. Ameacha watoto tisa na wajukuu 16.

No comments: