MWANAFUNZI IFM MBARONI KWA KILO 133.5 ZA MIHADARATI

Mwanafunzi wa mwaka wa Pili wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) pamoja na wengine wawili, wamekamatwa wakiwa na kilo 133.5 za bangi wakidaiwa kusafirisha Shinyanga kwenda Dar es Salaam.
Calvin Saleka (23) alikamatwa akiwa na mabegi mawili yakidaiwa kuwa na dawa hizo za kulevya kilo 51.
Wenzake ni John Joseph (31) mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam,  aliyekamatwa na kilo 42.5 na Joseph Charles (22), mkazi wa Shinyanga alikamatwa na kilo 36.5 za bangi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime aliwaambia waandishi wa habari jana mjini hapa kwamba kiasi hicho cha bangi, kinakadiriwa kuwa na thamani ya Sh milioni 20.
 Alifafanua mbinu waliyokuwa wametumia kufanikisha usafirishaji huo, ni kuhifadhi katika  mabegi makubwa ya nailoni kisha kusaga vitunguu na kuweka katika mabegi hayo pamoja na kupulizia manukato kuondoa harufu wasiweze kugundulika kirahisi.
Kwa mujibu wa Kamanda, watu hao walikamatwa juzi mchana eneo la stendi kuu ya mabasi ya mjini Dodoma baada ya kupanda basi kutoka kijiji cha Manonga-Tinde mkoani Shinyanga kwenda jijini Dar es Salaam.
Alitaja basi walilopanda ni la New Force, lenye namba za usajili T.931 CGU linalofanya safari  kati ya Kahama na Dar es Salaam. Walikamatwa kutokana na taarifa za raia waliowatilia shaka na kutoa taarifa Polisi.

No comments: