MWANACHUO AFIA KWA MPENZI AKIJARIBU KUTOA MIMBA

Mwanachuo wa Chuo cha Eden Hill (EDHICO) kilichopo mtaa wa Kwa Mfipa wilayani Kibaha mkoani Pwani, Attu Gabriel (miaka 18-19), amekutwa amekufa kwenye nyumba ya mpenzi wake, kwa kile kinachodaiwa kutaka kutoa mimba.
Awali, mwanafunzi huyo aliomba ruhusa kwenye uongozi wa chuo hicho Jumanne ya wiki hii kuwa anakwenda kumuuguza ndugu yake, aliyelazwa kwenye Hospitali ya Amana, Ilala jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kwamfipa, Emmanuel Kilasa, tukio hilo ni la jana saa 9 au 10 alfajiri nyumbani kwa mpenzi wake, Hafidh Mohammed (22) ambaye alikimbia baada ya tukio hilo.
Kilasa alidai Attu alipoomba ruhusa hiyo, alikuwa kwa mpenzi wake jirani na chuo hicho ambako alijaribu kutoa mimba, lakini hakufanikiwa.
"Tulipoingia kwenye chumba cha mpenzi wake, tulikuta kuna vitu kadhaa vikiwemo vidonge, chipsi, sukari na inasadikiwa kuwa alikuwa akijaribu kutoa mimba," alidai Kilasa.
Alidai kuwa mpenzi huyo wa marehemu, siku hiyo ya tukio, alikwenda kwa mama yake mzazi, Zaina Said na kumwambia kuwa alilala na mpenzi wake, lakini haamki.
"Mama yake alipofika, alimwambia kuwa  ameshakufa, hivyo aende akamwambie Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa, ndipo alipokimbia, kutokana na tukio hilo," alidai Kilasa.
Aidha, alisema baada ya tukio hilo, walitoa taarifa Polisi ambao walifika na kuuchukua mwili wa marehemu, ambaye alikuwa akiishi hosteli, nyumbani kwao ni Makambako mkoani Iringa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,  Ulrich Matei alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.
Alisema kwamba alikuwa hospitali, akifuatilia uchunguzi ili kujua chanzo cha kifo chake.

No comments: