MTUMBWI WAPINDUKA NA KUUA MWANAFUNZI KYELA

Watu wawili akiwemo mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Mwigo wilayani Kyela mkoani Mbeya, wanahofiwa kufa maji katika Mto Kiwira.
Hofu ya kufa maji watu hao inakuja baada ya mtumbwi waliokuwa wakiutumia, kupinduka.
Watu hao walikuwa wakitoka kijiji cha Ibungu kwenda kitongoji cha Ndandalo kilichopo Kyela. Mto huo unatajwa kujaa maji, kutokana na mvua nyingi zilizonyesha ukanda wa juu.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi baada ya kutokea ajali hiyo,  Mwenyekiti wa kitongoji cha Ndandalo, Lameck Mbembela alisema ajali hiyo ilitokea juzi  saa 10.30 jioni.
Mwenyekiti huyo alisema wakiwa katikati ya mto, mtumbwi uliyumba kutokana na udogo wake, ikilinganishwa na wingi wa maji yaliyokuwa yakitiririka kwa kasi.
Watu hao walitumbukia mtoni na katika  harakati za kujiokoa, watu watatu akiwemo mwongozaji walifanikiwa kujiokoa na kushindwa kuwaokoa wenzao,  ambao wanadaiwa hawakujua kuogelea.
Mbembela alitaja watu wanaosadikiwa kufa maji ni  Mzee Akupenda (70),  mkazi wa kijiji cha Ibungu na Stevin Stivin (15), mkazi wa Kyela, aliyekuwa anasoma kidato cha kwanza katika shule ya Sekondari Mwigo.
Mtoto huyo alikuwa akienda kumsalimia shangazi yake, anayeishi kitongoji cha Kyela Kati kilichopo ngÕambo ya mto huo.
Juhudi za kutafuta miili ya watu hao zinaendelea. Alitaka wananchi wanaotumia njia hiyo ya mitumbwi, waache na badala yake watumie njia kuu yenye daraja kubwa la kijiji cha Ipyana.
Mbembela aliitaka serikali kupitia halmashauri ya wilaya,  kujenga daraja katika mto huo, ambao hutumiwa na watu wengi  kufuata huduma za msingi mjini Kyela.

No comments: