MRADI WAPONGEZWA KWA KUPUNGUZA MAAMBUKIZI

Serikali imepongeza juhudi zilizofanywa na Mradi wa Champion  katika  kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Hayo yalisemwa jana na Mganga Mkuu wa Serikali, Donan Mmbando katika mkutano wa kufunga mradi huo uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema mradi huo ulioanzishwa mwaka 2008, umekuwa ukiwasaidia wanaume kujihusisha katika kupunguza maambukizi ya Ukimwi.
Alisema lengo ni kuongeza juhudi za kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo na utoaji wa elimu katika Kamati za Ukimwi katika ngazi zote.
“Kiwango cha maambukizi kimepungua kwa asilimia 18 mwaka 1988 hadi 5.1 kwa mwaka huu,” alisema Mmbando.
Alisema kazi kubwa wanayoifanya ni kuzuia maambukizi mapya,  kuhakikisha watu wote wanapata huduma na kuwasaidia wagonjwa katika upataji wa huduma.
Aidha alisema wamepata fursa ya kuzuia na kutibu kifua kikuu kwa waathirika na wameshirikiana na taasisi na asasi mbalimbali katika kuelimisha jamii.
Juhudi nyingine ni kutoa elimu kuhusu tohara kwa mikoa yenye maambukizi makubwa ya Ukimwi, utokomezaji wa maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Katika maoni yake, Mkuu wa Championi,  Jane Schueller alisema mradi  ulizinduliwa Februari 2008 na watu wa Marekani na kuungwa mkono na Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani (USAID).
Alisema watu 345,000 wamefikiwa na mradi wa kupambana na Ukimwi na Afya ya Uzazi na wengine  260,000 walifikiwa na mradi huo kwa kupewa elimu dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.
Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti  Ukimwi (Tacaids), Fatma Mrisho alisema mradi huo umeleta usawa wa jinsia katika jamii na kuhakikisha wanaume wanakuwa karibu katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

No comments: