MKUU WA WILAYA ILALA ATAKA WATENDAJI KUWA WAAMINIFU

Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Raymond Mushi amewataka watendaji wa kata, mitaa na wenyeviti , kutanguliza mbele suala la uaminifu katika ukusanyaji kodi za majengo ili kuiwezesha wilaya hiyo kufikia Malengo ya Matokeo Makubwa  Sasa (BRN).
Mushi alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam juzi, alipofungua semina ya siku moja ya watendaji na wenyeviti hao kutoka Tarafa ya Ukonga, iliyokuwa na lengo la kuwapa elimu juu ya suala zima la ukusanyaji wa mapato hayo.
Alisema ili kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia mia moja yaliyowekwa na wilaya hiyo, kila mtendaji hana budi kujipima kutokana na utendaji wake hatua aliyosema pia itamsaidia kutoa elimu kwa wananchi wanaomzunguka katika eneo lake.
“Nyinyi kama viongozi  mnapaswa kujituma ili malengo yaweze kufikiwa na kubwa zaidi itakuwa vizuri kama mtaweka mbele suala la  uaminifu wakati wa ukusanyaji wa mapato hayo vinginevyo hakuna mafanikio yoyote yanayoweza kufikiwa,” alisema Mushi.
Aidha alisema malengo ya wilaya hiyo ni kuongoza katika maeneo mbalimbali dhidi ya wilaya zingine zote na hivyo kuwa mfano jambo alilosema litafanikiwa  kama viongozi hao watajituma na kuzingatia ushauri unaotolewa kwao.
“Tunataka wilaya yetu iwe ya mfano katika ulinzi na usalama ili watu waweze kuishi kwa amani, hivyo ili iwe salama ni vizuri kuwandaa watu kuanzia sasa kwa kuwa thamani ya mtu hupanuka kwa kuongeza upeo wake tuna kila sababu kutia mkazo katika suala hili la Matokeo Makubwa Sasa kielimu ili tufike huko,” aliongeza Mushi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Fedha kutoka wilaya hiyo, Stellah Mgumia aliwataka watendaji na wenyeviti hao kusimamia vyema suala zima la ukusanyaji wa mapato ili kuiwezesha wilaya hiyo kufikia malengo waliyojiwekea.
Alisema lengo la Serikali kurejesha suala la ukusanyaji kodi za majengo katika halmashauri, lilitokana na maombi yaliyokuwa yametolewa na halmashauri hizo, hivyo wanapaswa kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuonesha kwa vitendo dhamira yao ya kulitaka hilo.
Alisema ni jambo la fedheha kuiona baadhi ya mitaa inasuasua katika ukusanyaji wa kodi hizo, jambo alilosema linatia shaka kufikiwa kwa malengo waliyojiwekea.

No comments: