MKUU WA UPELELEZI AUAWA KWA KUCHOMWA KISU SHINGONI

Mkuu wa Upelelezi, Kituo cha Polisi Isebania Wilaya ya Kurya West, Kenya kilicho mpakani na Tanzania,  John  Kaduri ameuawa kwa kuchomwa kisu shingoni na mtuhumiwa wa vitendo vya uhalifu.
Mtuhumiwa huyo, Simon Mkisii maarufu kama Rasta,  pia aliuawa na wananchi baada ya tukio hilo.
Mtu huyo alikuwa akisakwa na polisi wa Kenya, akituhumiwa kujeruhi watu kadhaa kwa kisu na panga wakati wa sikukuu ya Pasaka.
Akisimulia tukio hilo, Mkuu wa Kituo cha Isebania, Juma Kwomba alisema mauaji hayo ya polisi yalifanyika Aprili 24 jioni katika mji huo wa Isebani.
Kwomba alisema yeye si msemaji wa jeshi hilo Kenya, lakini alisimulia kilichojiri. Alisema siku hiyo ya tukio polisi aliyeuawa (Kaduri), akiwa kazini alipata taarifa juu ya kuonekana mtuhumiwa  Mkisii. 
"Inspekta John  Kaduri alimkaribia mtuhumiwa, alipotaka kumweka chini ya ulinzi, mtuhumiwa Rasta alimrukia na kumchoma kisu shingoni,” alisema.
Alisema, “Kaduri aliomba msaada na jeshi letu lilifika haraka na kumchukua na kumkimbiza Hospitali ya Ombo Migori (Kenya) katika juhudi za kutaka kuokoa maisha yake,  lakini alikufa kabla ya kupatiwa matibabu.”
Inasadikiwa mtuhumiwa alikimbilia Kituo cha Polisi, lakini umati wa wananchi wenye hasira walimfuata, wakimfukuza kwa mawe na kumshambulia hadi alipopoteza maisha nje ya Kituo cha Polisi Isebania.
Maeneo ya mpaka huo wa Sirari upande wa Tanzania na Isebania, Kenya,  yanadaiwa kukumbwa na  matukio ya uhalifu ya mara kwa mara, ikiwemo kushambulia maofisa wa polisi.

No comments: