MKAZI WA SINZA AUNGUA MOTO USONI HADI MIGUUNI

Mkazi mmoja wa eneo la Sinza jijini Dar es Salaam, amejeruhiwa vibaya baada ya chumba chake kuteketea kwa moto uliozuka ghafla.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema jana kuwa tukio hilo ni la juzi saa 2:00 asubuhi eneo la Sinza A kwenye nyumba Namba 426, yenye vyumba nane inayomilikiwa na Elizabeth Kilali.
Kamanda Wambura alisema moto huo ulizuka ghafla katika chumba cha mpangaji huyo, Mariam Kabaka ambaye aliungua kuanzia usoni hadi miguuni kwa moto huo. Alisema moto huo uliteketeza chumba chote cha mtu huyo.
Alisema chanzo cha moto huo ni  jiko la gesi, alilowasha chumbani kwake kupika uji,  ambapo mtungi wa jiko hilo la gesi, ulilipuka na kuwaka moto.
"Majeruhi huyo ameungua kuanzia usoni hadi miguuni na kumsababishia majeraha, kwa sasa amelazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na moto huo ulizimwa na Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji cha Jiji wakisaidiana na wananchi," alisema Kamanda Wambura.
Katika tukio jingine Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo alisema kuwa katika msako uliofanywa na askari Mbagala, walifanikiwa kuwakamata watu saba wakiwa na bangi puli mbili na kete 32.

No comments: