MICHE 500 YA KARAFUU YAPANDWA UNGUJA NA PEMBA

Zaidi ya miche ya karafuu 500,000 imepandwa Unguja na Pemba katika kipindi cha mvua za masika zinazoendelea nchini kote.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Maliasili, Dk Juma Abdallah alisema hayo wakati alipozungumza na gazeti hili juu ya mikakati ya kuotesha karafuu nyingi zaidi katika kipindi hiki.
Alisema mvua za masika  ni nzuri kwa wakulima kwa ajili ya kupanda miti ya aina mbalimbali ikiwemo ya karafuu na matunda.
"Tunawaomba wakulima wa Unguja na Pemba kupanda mikarafuu mingi zaidi katika kipindi hiki cha mvua za masika zinazoendelea kunyesha," alisema.
Abdallah alisema Serikali imechukua juhudi za kuimarisha vitalu vya kuotesha karafuu, Unguja na Pemba kwa ajili ya kusambaza kwa wakulima bure.
Jumla ya vitalu vya kuotesha karafuu 20 vimeimarishwa Unguja ikiwemo Kizimbani, Mwera, Machuwi pamoja na Kiyanga.
Aidha alisema kazi kubwa inayofanywa na Wizara ya Kilimo kwa sasa ni kuwaendeleza mabibi shamba na mabwana shamba kwa ajili ya kutoa elimu ya kuendeleza kilimo cha karafuu.
"Wizara ya Kilimo na Maliasili imesambaza mabibi shamba na mabwana shamba wilaya zote za Unguja na Pemba kwa ajili ya kutoa elimu juu ya mbinu sahihi za kuendeleza kilimo cha mafanikio," alisema.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ipo katika mikakati ya kuimarisha zao la karafuu ikiwemo juhudi za kuotesha miche mingi ya karafuu hadi kufikia milioni moja kwa mwaka.

No comments: