MFUKO WA SEKTA BINAFSI WAZINDULIWA

Rais Jakaya Kikwete amezindua mfuko wa sekta binafsi wa kuwezesha wawekezaji nchini katika kupata mtaji, utakaokuza biashara na kukuza uchumi nchini.
Mfuko huo unajulikana kama Mkoba, unalenga kutoa mitaji inayoanzia dola milioni moja hadi milioni 15.
Hafla ya uzinduzi huo, ilifanyika jana Dar es Salaam ambapo Rais Kikwete alisema ujio wa mfuko huo ni fursa kubwa itakayosaidia kutoa mitaji haswa kwa wajasiriamali wadogo . Iliandaliwa na Taasisi  Uongozi Institute na Mkoba.
Alisema nchi yoyote inayokua kiuchumi husaidiwa na sekta binafsi ambao hupatiwa mitaji yenye kukuza biashara zao katika mazingira yaliyo nafuu.
“Mashirika mengi ya sekta binafsi hutegemea sana mikopo kutoka katika taasisi za fedha ili kuboresha biashara zao ambayo riba yake huwa kubwa," alisema na kuongeza kuwa mkoba umekuja kwa wakati muafaka.
Alisema Tanzania ni moja ya nchi za Afrika inayokua kiuchumi, jambo ambalo
linapanua wigo wa biashara pamoja na kuongeza  wawekezaji  kutoka nje ya nchi.
Rais Kikwete alisema kuingia kwa mkoba nchini, kunaleta ushindani katika kuzalisha bidhaa  na kuongeza masoko kwa biashara za ndani zitakazopelekea kukua kwa kampuni kwa kiwango kikubwa.
“Uwezo wa kupata fedha ni changamoto kubwa nchini kwa wajasiriamali wengi wadogo na kuja kwa mkoba ni njia madhubuti ya kukuza uchumi ambao kwa sasa umekuwa kwa asilimia saba,” alisema .
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mkoba, Dk Frannie Leautier alisema  mfuko huo utawezesha mitaji kwa wawekezaji na lengo kubwa ni kukuza uchumi kwa nchi za Afrika.
Alisema wajasiriamali wadogo na wa kati  wamekuwa wakizalisha ajira na kukuza uchumi ingawa wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya mtaji.
“Ujio wa mkoba ni mahsusi kwa kuitoa pengo lililopo la kukua kibiashara kwa kuwa na wigo wa kupata mitaji kwani zipo baadhi ya biashara ambazo zinashindwa kukua kwa kukosa uwezo wa kifedha,” alisema Leautier.
Dk Frannie alisema mkoba inatarajia kuwa na dola milioni 300  ambazo zitawekezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo nishati, ubunifu ili kuwezesha maendeleo yenye kukuza uchumi.

No comments: