MASSAWE MGENI RASMI TAMASHA LA BUGANGUZI

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fabian Massawe kesho anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tamasha lililoandaliwa na wakazi wa Kata ya Buganguzi, wilayani  Muleba likilenga pamoja na masuala mengine, kuchangia ujenzi wa kituo cha afya.
Wakazi hao walioamua kuchangishana fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya  kitakachogharimu zaidi ya Sh milioni 500, kesho wanatarajiwa kukutana chini ya uratibu wa Chama cha Maendeleo ya Kata ya Buganguzi (BUGADEA) katika tamasha maarufu kama ‘Buganguzi Day’.
Makamu Mwenyekiti wa Bugadea, Alex Mutiganzi, aliliambia mwandishi hivi karibuni  kwamba Massawe  amethibitisha kushiriki tamasha hilo litakalofanyika makao makuu ya kata hiyo, Katare, likiambatana na harambee ya kuchangia kituo hicho cha afya.
Bugadea ambacho waasisi wake ni wakazi wa kata hiyo waishio Dar es Salaam,  chini ya uenyekiti wa Rodrick Lutembeka, ndio waratibu wa michango ya ujenzi. Kata hiyo iliyo katika Tarafa ya Nshamba, ina vijiji vya Buhanga, Bushemba, Katare na Kashozi.
Kwa mujibu wa Mutiganzi,  katika kuhakikisha wanaunganisha wananchi kimaendeleo,  kila mwaka Bugadea huandaa tamasha hilo ambalo hufanyika kila Jumamosi ya Pasaka kujadili mambo ya maendeleo ikiwemo ujenzi huo wa kituo.
Alisema wameamua kata iwe na kituo cha afya kupanua wigo wa huduma za afya na kuondoa kero ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata hospitali kubwa.
Bugadea kwa kushirikiana na uongozi wa kata, waliamua kuanza ujenzi kwa kuweka msingi; lengo likiwa ni kujenga wadi nne zitakazowezesha kulaza wagonjwa wapatao 40 kwa pamoja.
“Hadi tulikofika, ni michango ya wananchi wenyewe,” alisema Mutiganzi. Akihimiza  wazawa wa kata hiyo  na zilizo jirani kuchangia ujenzi, Mutiganzi alisema Halmashauri ya Wilaya ya Muleba imeahidi kuchangia Sh milioni 60.

No comments: