MASHARTI YA THELUTHI MBILI KUKWAMISHA KATIBA MPYA

Hofu ya kutopatikana kwa Katiba mpya, baada ya changamoto zilizojitokeza wakati wa awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba, sasa ni dhahiri.
Hofu hiyo inaonekana katika mahojiano maalumu kati ya waandishi wa HabariLEO na Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad.
Katika mazungumzo kuhusu nini anafikiri kinafaa kufuatwa kwa sasa baada ya hekaheka ya awamu ya kwanza, Katibu huyo alipendekeza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ifanyiwe marekebisho.
Katibu huyo katika mazungumzo, amesema kama msimamo wa wajumbe wa Bunge hilo waliojiundia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), utaendelea kuwa kama ulivyo, mchakato wa kupata Katiba mpya kwa Sheria iliyopo, unaweza kuganda.
Kutokana na hali hiyo, amependekeza kwa maoni yake binafsi kwamba ni vyema Serikali ifikirie kubadilisha Sheria hiyo kwa kurekebisha masharti yanayotaka kila kifungu cha Katiba hiyo, kipite baada ya kupigiwa kura na zitakazounga mkono za theluthi mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe kutoka Zanzibar.
Kwa mujibu wa kifungu cha 26(2) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ili Katiba inayopendekezwa ipitishwe katika Bunge Maalum la Katiba, itahitaji kuungwa  mkono kwa wingi wa theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge Maalum kutoka  Tanzania Bara, na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.
Hata hivyo Katibu huyo alisema ipo haja kwa Serikali kurekebisha kifungu hicho, kwa kuwa kama wajumbe wa Ukawa waliosusia vikao vya Bunge hilo na kutoka nje Aprili 16 mwaka huu wataendeleza msimamo wao, Katiba itaganda.
“Kubadili theluthi mbili mimi siwezi kulisemea maana ni kazi ya Serikali, lakini ni vizuri likaangaliwa, hatuwezi kuganda kwa mbili ya tatu (thelithi mbili),” alisema Katibu huyo.
Alisema wajumbe hao wa Ukawa wengi ni wa vyama vya siasa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na wanashirikisha pia baadhi ya wajumbe wa kundi la 201 wasiozidi 25.
Hata hivyo alisema: “Bado tunaendelea kuwaomba wajumbe waliotoka bungeni waje tufikie mwisho wa jambo hili kwa maslahi ya Taifa.”
Alipendekeza marekebisho ya Sheria yafanyike, na badala ya kusema theluthi mbili ya akidi ya wajumbe wote, ni bora iseme theluthi mbili ya wajumbe waliohudhuria vikao wakati uamuzi ukifanyika.
Hata hivyo, mabadiliko ya Sheria hiyo yatalazimisha kufanyike mabadiliko ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, kwa kuwa imezuia baadhi ya vipengele visifanyiwe uamuzi, isipokuwa uamuzi huo uungwe mkono na idadi ya kura ya theluthi mbili ya wabunge kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wabunge kutoka Zanzibar.
Zuio hilo lipo katika Orodha ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na limetajwa katika Ibara 98 (1) (b)  kwa kuorodhesha mambo ambayo mabadiliko yake yatahitaji masharti hayo.
Mambo hayo ni kuwapo kwa Jamuhuri ya Muungano, kuwapo kwa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano, kuwapo kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano, madaraka ya Serikali ya Zanzibar, Mahakama Kuu ya Zanzibar na Orodha ya Mambo ya Muungano. 
Pamoja na Bunge Maalumu kuendelea kutafuta suluhu ili wajumbe hao wa Ukawa warejee bungeni, Katibu huyo wa Bunge Maalumu, aliweka wazi namna wajumbe hao walivyokuwa na msimamo mgumu wa kuendelea kususia Bunge Maalumu.
Kuhusu kikao cha Kamati ya Uongozi kilichokaa Alhamisi iliyopita, Katibu alisema pamoja na mambo mengine kilipokea taarifa ya Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta ya kwenda Zanzibar kukutana na baadhi ya viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Ukawa kutafuta suluhu ili wajumbe hao warejee.
Viongozi wa Mapinduzi Zanzibar aliokutana nao Sitta ni pamoja na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, Rais mstaafu, Amani Abeid Karume na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad.
Kwa mujibu wa Katibu huyo, ziara ya Sitta visiwani humo aliyoifanya Jumatatu ya wiki iliyopita, ililenga kutafuta suluhu ya wajumbe waliotoka bungeni kurejea tena, lakini viongozi wa Ukawa kutoka vyama mbalimbali vya siasa, ambao pia ni wajumbe wa Bunge hilo na wasio wajumbe, waligoma ombi la Sitta kuwataka warejee mpaka wapate ridhaa ya vyama vyao.
“Mwenyekiti alikwenda Zanzibar kukutana nao (Ukawa) na wajumbe hao walisema hawawezi kuzungumza na Sitta kuhusu kurudi mpaka wapate uamuzi wa vyama vyao, baadhi ya viongozi aliwapigia simu lakini walipokea wasaidizi wao na alipowaambia wahusika wakipata ujumbe wake wampigie, hakuna aliyepiga,” alieleza Katibu.
Alisema wajumbe wengine Sitta aliwatumia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, akiwaomba waongee naye lakini hawakujibu.
Hata hivyo Katibu alisema bado Sitta ana matumaini kwamba watarejea na anaendelea na juhudi za kutafuta mapatano.
Ingawa Ukawa hawakutaka kupokea simu wala kujibu ujumbe mfupi wa maneno waliotumiwa na Sitta, lakini baadhi yao walionekana kurejea kufuata posho kimya kimya bungeni humo na idadi yao imeelezwa kuwa ni zaidi ya 10.  Hata hivyo hawakupewa posho za kuanzia Aprili 19 hadi 26.
Katibu alipoombwa kuwataja majina, aligoma kutoa  kwa kile alichoeleza kuwa ni kwa matumizi ya ofisi pekee kwa kuwa bado wanaendelea na uchunguzi wa suala hilo.
Alisema hoja iliyotolewa na Mjumbe Said Mkumba   kwamba Ukawa walirejea kuchukua posho, ilitawaliwa na hofu na kujisemea tu, kutokana na ukweli kwamba, wajumbe hao walipaswa kuchukua posho zao za vikao za mpaka Aprili 18.
Aprili 17 baada ya wajumbe wa Ukawa kutoka nje ya Bunge, mjumbe Mkumba alikaririwa bungeni akidai kuwa Ukawa walirejea na wameonekana kwa mhasibu wakidai posho zao zote, jambo lililoelezwa na Katibu kuwa halikuwa sahihi lakini liliwalazimu kubadilisha utaratibu.
“Kutokana na tukio la Ukawa, ingawa wamo wachache walibaki bungeni, ilibidi tuzingatie utaratibu wa mtu aliyefika kwenye kikao ndio anasaini na kulipwa, ama la akiwa na dharura, alete maelezo ya Mwenyekiti kuhusu dhahura yake,” alisema Hamad na kuongeza kuwa walifanya hivyo baada ya kubaini baadhi ya Ukawa waliotoka, walirejea kuchukua posho.
Kuhusu nyongeza ya siku 60, Katibu alisema ipo kwa mujibu wa sheria baada ya mabadiliko yaliyofanyika Februari mwaka huu kuondoa kipengele cha nyongeza ya ukomo wa siku 20 baada ya siku 70 kumalizika.
Kifungu hicho ni 28 (4) kinachotoa mamlaka kwa Mwenyekiti na Makamu wake kuongeza siku kwa ridhaa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, bila kuathiri kifungu cha 28 (3) kinachoeleza siku 70 za awali.

No comments: