MAMLAKA YA BANDARI WASAINI MKATABA NA WABELGIJI

Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imesaini mkataba na Kampuni ya Phaeros Group ya nchini Ubelgiji kwa ajili ya kuanza mradi wa kielektroniki, unaotumia mfumo wa ‘Electronic Single Windows System’.
Mkataba huo ulisainiwa juzi Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano wa TPA, Phares Magesa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Stan De Smet mbele ya wadau wakuu wa usafirishaji.
Akizungumzia mfumo huo, Magesa alisema hiyo ni moja ya kutekeleza mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambapo lengo kuu ni kurahisisha usafirishaji wa bidhaa kutokana na mfumo huo utapunguza mizigo na meli zinazochelewa kuhudumiwa na kutolewa bandarini hapo.
“Tunataka kuhakikisha ndani ya siku tano baada ya mfumo huu kuanza kutumika  mzigo uwe umeshatoka, inaweza ikachukua siku moja au mbili lakini lengo letu isizidi siku tano,” alisema Magesa.
Alisema mfumo ambao utaanza Juni, mwaka huu kwa majaribio unatarajiwa kupunguza gharama za ziada na muda wa usafirishaji, kwa kuanzia mfumo huo utaanza katika bandari ya baharini na baadaye katika bandari kavu.
Alisema kwa sasa bandari hiyo inapokea tani milioni 13 kwa mwaka, lakini baada ya mfumo huo kuanza kufanya kazi wanategemea kwa mwaka huu kufikisha tani milioni  15 na mwakani tani milioni 18.
“Jumla ya gharama zote ukijumuisha ununuzi wa mdumo wenyewe na gharama zingine inaweza kufikia dola za Marekani milioni 17 au 18,” alisema.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi wa mfumo huo, Jumbe Menya alisema mfumo huo utaongeza ushindani wa kibiashara na katika nchi za Afrika Mashariki. Tanzania ni ya kwanza kuwa na mfumo huo katika bandari za baharini.

No comments: