MAKOSA YA USALAMA BARABARANI YAINGIZIA SERIKALI SHILINGI MILIONI 144.5

Polisi  Kanda Maalumu ya Dar es Salaam imekusanya Sh milioni 144.5 katika kipindi cha wiki moja kutokana na makosa mbalimbali ya usalama barabarani ikiwemo yaliyosababishwa na pikipiki.
Jumla ya pikipiki 526 tayari zimeshakamatwa kutokana na makosa mbalimbali, ikiwemo kuingia katika eneo la katikati ya jiji licha ya kupigwa marufuku.
Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari juzi wakati akitoa taarifa mbalimbali kuhusiana na hali ya usalama wa jiji hilo kuwa mbali na pikipiki hizo pia wamekamata magari 3028, daladala 1,950  na malori 1,078.
"Hiki ni kiwango kilichopatikana ndani ya wiki moja lakini hii itakuwa ni operesheni endelevu ili kuhakikisha sheria za usalama barabarani zinafuatwa," alisema Kova.
Aidha alitaka madereva wote kutii sheria bila shuruti hasa katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Pasaka kutokana na maeneo yote ya jiji hilo kuwa na ulinzi mkali.

No comments: