MAKOSA 288 YARIPOTIWA OFISI YA TAKUKURU MBEYA

Makosa  288 yanayohusu malalamiko ya rushwa yaliripotiwa katika ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkaoni Mbeya  kuanzia Januari hadi Desemba mwaka jana.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora, George Mkuchika aliyasema hayo jana mjini hapa alipokuwa akizungumza na wajumbe wa Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Mbeya (RCC) kwa lengo la kutoa elimu ya utawala bora kwa wajumbe hao.
Mkuchika alitaja Serikali za Mitaa kuongoza kwa kuwa na malalamiko 65 ikifuatiwa na Idara ya Mahakama iliyokuwa na malalamiko 46 huku Idara za Polisi na sekta binafsi zikiwa na malalamiko 35 kila moja.
Alisema kutoka halmashauri kulikuwa na malalamiko 18,Tanesco kulikuwa na malalamiko matatu huku Idara za Uhamiaji, Maliasili, Serikali Kuu, vyombo vya habari, taasisi za dini na Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ) zilikuwa na lalamiko moja kila moja.
Waziri huyo alisema bado kuna ushirikiano mdogo wa wadau katika kukabili rushwa. Alitaka jamii ibadilike na kutoa ushirikiano wa kutosha badala ya kuachia wizara na Takukuru pekee.
Wajumbe wa kikao hicho waliomba kubadilishwa kwa sheria ya Takukuru ili  iweze kuipa meno taasisi hiyo kwa kuruhusu kuchunguza na kushitaki yenyewe pasipo kupeleka mashitaka kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) hatua waliyosema imekuwa ikichelewesha uendeshaji wa mashitaka.
Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Chrispin Meela aliitaja wilaya yake kuwa miongoni mwa maeneo nchini ambayo kuna mashitaka mengi ya Takukuru ambayo hayakuweza kuendeshwa kutokana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka kuchelewa kurejesha majibu.

No comments: