MAGEREZA WAOMBA NDUGU WA MAHABUSU WALIOFARIKI AJALINI

Miili ya mahabusu wanne waliokufa katika ajali iliyotokea juzi wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, inasubiri kutambuliwa na ndugu kwa ajili ya kuendelea na maziko.
Kamishna wa Magereza, John Minja alitoa pole kwa familia za mahabusu  hao wanne pamoja na  askari magereza mmoja waliokufa katika ajali hiyo.
"Natoa pole kwa familia zilizopatwa na msiba huo au kuguswa kwa namna yoyote, hiyo ni mipango ya Mungu hatuwezi kubadilisha na ni ajali ya kawaida kama ajali nyingine, taratibu nyingine zinaendelea kuhakikisha miili yote inatambuliwa na ndugu na kuchukuliwa," alisema Kamishna Minja.
Waliokufa katika ajali hiyo papo hapo ni askari magereza Sajini Peter Mabuma, mahabusu waliokufa ni Juma Mohamed (19), Faraja Msahamu (40), Alex Athumani (23) na Hamis Juma (38).
Mahabusu hao walikuwa wanatoka Mahakama ya Mwanzo Kimanzichana kupelekwa Gereza la Keko, jijini Dar es Salaam.
Kamishna Minja alisema ndugu za mahabusu watachukua miili kwa maziko.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Ulrich Matei, alisema ajali hiyo ilitokea baada ya gari lililokuwa limewabeba mahabusu hao, lenye namba za usajili MT 0038, kuligonga lori lililokuwa limeegesha barabarani na kupinduka. 
Kamanda Matei alilitaja lori hilo lenye namba za usajili T446 CJS lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara katika Kijiji cha Kinene Mwalusembe, wilayani humo.
Gari lililowabeba mahabusu lilikuwa likiendeshwa na Koplo Zawadi Makupa (41) ambaye anashikiliwa na Polisi.
Askari aliyepata majeraha kichwani na kwenye mikono yote miwili, B 2977 koplo Mohamed  hali yake ilikuwa mbaya akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH). Ilielezwa hali yake siyo nzuri.

No comments: